Kiungo wa Brighton kutoka Zambia, Enock Mwepu, astaafu mapema kufuatia ugonjwa wa moyo

Mwepu alisema uamuzi wa kustaafu unafuatia ushauri ambao alipatiwa na wataalamu wa afya.

Muhtasari

•Taaluma ya Mwepu imekatizwa na ugonjwa wa kurithi wa moyo, klabu ya Brighton amefichua katika taarifa yake.

•Mwepu alitoa shukrani za dhati kwa klabu yake na wote ambao wamefanikisha taaluma yake ya kandanda.

Kiungo wa Brighton Enock Mwepu aking'ang'ania mpira na Kevin De Bruyne wa Manchester City katika mechi ya awali.
Image: TWITTER// ENOCK MWEPU

Mchezaji kandanda wa kimataifa wa Zambia Enock Mwepu ametangaza kustaafu mapema kufuatia masuala ya kiafya.

Katika taarifa aliyotoa Jumatatu, kiungo huyo wa kati ambaye anachezea klabu ya EPL ya Brighton & Hove Albion alisema uamuzi wa kustaafu unafuatia ushauri ambao alipatiwa na wataalamu wa afya.

"Ndoto zingine huisha, kwa hivyo ni kwa huzuni kwamba ninatangaza hitaji la kustaafu kwa sababu ya ushauri wa matibabu ambao nimepokea. Walakini huu sio mwisho wa kujihusisha kwangu na mpira wa miguu, ninapanga kuendelea kuhusika katika nafasi fulani," alisema kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Mchezaji huyo alitoa shukrani za dhati kwa klabu yake na wote ambao wamefanikisha taaluma yake ya kandanda.

Taaluma ya Mwepu imekatizwa na ugonjwa wa kurithi wa moyo, klabu ya Brighton amefichua katika taarifa yake.

Klabu hiyo imefichua kuwa familia ya Mwepu imekuwa ikipitia kipindi kigumu tangu mwanasoka huyo alipogunduliwa na ugonjwa huo wiki chache zilizopita.

"Kama klabu tutampa upendo, msaada na usaidizi wote tuwezavyo ili kupata afueni kamili, na kisha anapoamua kuhusu hatua zinazofuata maishani mwake," Mwenyekiti wa klabu hiyo Tony Bloom alisema.

Enock aliugua akiwa kwenye ndege akielekea kuungana na kikosi cha Zambia wakati wa mapumziko ya kimataifa na baada ya kukaa hospitalini nchini Mali kwa muda alirejea Brighton kufanyiwa vipimo zaidi vya moyo na huduma zinazoendelea.

Vipimo vilibaini kuwa ugonjwa wake ni kutokana na hali ua kurithi ya moyo, ambayo hujitokeza baadaye katika maisha na haikuonekana hapo awali kwenye uchunguzi wa kawaida wa moyo.

Inasemekana kuwa hali hii inaweza kuwa mbaya zaidi kwa kucheza michezo hivyo Enock ameshauriwa kuwa chaguo pekee kwa ajili ya usalama wake ni yeye kuacha kucheza soka.