HALI YA WASIWASI

Mbappé atishia kuvunja uhusiano na Paris Saint-Germain

Tukio hilo linajiri miezi minne tu baada ya nyota huyo kusaini mkataba mpya.

Muhtasari

•Mbappé anasemekana kukasirishwa na uamuzi wa kumchezesha kama nambari 9 badala ya nafasi yake anayopendelea wa upande wa kushoto.

•Mbappé alitarajiwa kuondoka PSG na kujiunga na Real Madrid msimu uliopita lakini aliwashangaza wengi alipokataa ofa ya klabu hiyo ya Uhispania.

Kylian Maple akionyesha tuzo lake la mchezaji bora katika mechi yao ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Benfica.
Kylian Maple akionyesha tuzo lake la mchezaji bora katika mechi yao ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Benfica.
Image: HISANI

Mshambuliaji aliyeshinda Kombe la Dunia Kylian Mbappé anaripotiwa kutokuwa na furaha katika klabu yake ya Paris Saint-Germain na ameeleza nia ya kuondoka Januari.

Tukio hilo linajiri miezi minne tu baada ya nyota huyo kusaini mkataba mpya ambao ulikusudiwa kumweka Parc des Princes hadi 2025.

Ripoti kutoka kwa vyombo mbalimbali vya habari vya Ufaransa zilionyesha kwamba mabingwa hao wa Ligue 1 hawana nia ya kumwachilia fowadi huyo mwenye umri wa miaka 23.

Mbappé anasemekana kukasirishwa na uamuzi wa kumchezesha kama nambari 9 badala ya nafasi yake anayopendelea wa upande wa kushoto.

PSG wanaamini kwamba Mbappé ameruhusu kutoridhika kwake kujulikana ili kuweka shinikizo lakini klabu hiyo imesema inakusudia kukataa ofa yoyote kwa mchezaji huyo.

Mbappé alitarajiwa kuondoka PSG na kujiunga na Real Madrid msimu uliopita lakini aliwashangaza wengi alipokataa ofa ya klabu hiyo ya Uhispania.

Mbappé amefunga mara 11 katika mechi 12 msimu huu na PSG kwa sasa ipo kileleni mwa jedwali kwa kushinda mara nane na kuandikisha sare mbili katika mechi 10.

Hata hivyo, mkurugenzi wa michezo wa Paris Saint-Germain Luis Campos amekanusha madai kwamba Kylian Mbappe ameomba kuondoka katika klabu hiyo mwezi Januari.

“Niko hapa kukana waziwazi, yeye (Mbappé) hakuzungumza nami au na rais wangu kuhusu kuondoka Januari. Swali hili halikutokea na hatukuwahi kulizungumzia. Kuna uvumi kila siku, na hatuwezi kuzungumza juu yao kila siku. Lakini hii, ni mbaya. Maana jina langu lipo. Athari kwenye chumba cha kufuli? Hapana, ni wachezaji wazoefu. Walakini, sio habari ya kweli, na haitavuruga kikundi.

“Tunazungumza na Kylian kila siku, kama vile Neymar, Danilo, Vitinha na Verratti. Wachezaji wote wana mawazo yao na tunajadili. Juu ya kuajiri, tulizungumza juu yake mwezi mmoja uliopita. Ilikuwa wazi sana. Na leo, tunafanya kazi kila siku kuwa na nguvu zaidi,” aliambia chombo cha habari cha Canal.

Mbappé alitawazwa mchezaji bora wa mechi katika sare ya 1-1 kwenye mechi yao ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Benfica siku ya Jumanne.

Sasa ndiye mfungaji bora wa muda wote wa Paris Saint-Germain kwenye UEFA Champions League akiwa amefunga mabao 31.

Paris Saint-Germain na Benfica zote zilikosa nafasi ya kutinga hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, zikiwa zimesalia mechi mbili kutokana na sare hiyo katika mji mkuu wa Ufaransa.

Wawili hao walisawazisha matokeo ya mkutano wao mjini Lisbon wiki iliyopita, na kuwaacha wakiwa wameambulia pointi nane kila mmoja kutokana na michezo minne ya Kundi H.