Alianza Mourinho, Zlatan, Pogba na sasa Ronaldo, kunani Man United?

Kauli ya Ronaldo kuhusu kusalitiwa na United ndiyo msumari wa mwisho kwenye uhusiano wake na klabu.

Muhtasari

•Ronaldo ameisema vibaya United, kwenye maeneo mengi ikiwemo matumizi ya teknolojia za muda mrefu, kutomuheshimu na mfumo wa maisha wa klabu.

•Pogba alivyoondoka na yeye hakuzungumzia vizuri maisha yake Old Trafford.

Image: BBC

Uchumba wa Cristiano Ronaldo na Manchester United uko mashakani. Kauli yake kuhusu kusalitiwa na klabu hiyo ndiyo msumari wa mwisho kwenye uhusiano huo.

Ingawa mahojiano yake na mwandishi Piers Stefan Pughe-Morgan hayajatoka rasmi, yakitarajiwa kutoka wiki hii, vipande vya mahojiano haya vilivyoachiwa Jumapili na Jumatatu vimeibua mjadala mkubwa.

Hoja za Ronaldo ni nyingi kuhusu United. Kwa ujumla ameisema vibaya United, kwenye maeneo mengi ikiwemo matumizi ya teknolojia za muda mrefu, kutomuheshimu na mfumo wa maisha wa klabu.

Mchambuzi na mchezaji wa zamani wa Simba na timu ya taifa ya Tanzania, taifa stars, Amri Kiemba aeiambia BBC kwamba Ronaldo 'anapumua' baada ya kubanwa na mambo mengi klabuni hapo.

'Tusisahau ni binadamu kama binadamu wengine'.

Kauli za Ronaldo na zingine kuhusu kuendeshwa kizamani, kutojali hisia za wachezaji, matokeo na mafanikio ya timu zaidi ya mafanikio ya mapato, zinarejesha kauli nyingi za zamani zilizowahi kutolewa na kocha na wachezaji waliowahi kujtokeza hadharani. Na hilo linaleta maswali mengi, lakini kubwa zaidi, je kuna ni Man United?

Uendeshaji wa klabu

Kama ilivyo kwa vilabu vingine vikubwa duniani, mfumo wa uendeshaji wa Manchester hautofautiani sana, unaundwa na bodi, watendaji na timu. Ni moja ya timu zenye mafanikio makubwa kibiashara na uwanjani. Ikiwa na rekodi ya mataji 20 ya ligi na kuwa miongoni mwa vilabu tajiri duniani.

Kwa sasa inamilikiwa nwa watoto 6 wa mzee Malcom Glazer ambao ni Avram, Joel, Kevin, Bray, Darcie na Edward, ambao baada ya baba yao kufariki mwaka 2014, asilimia 90 ya hisa za umiliki wa klabu wakagawana kwa usawa.

Joel na Avram wakiwa na majukumu ya kila siku ya usimamizi wa klabu tangu mwaka 2006 baba yao alipoanza kuugua. Wanaungana sasa na wengine kina Kevin, Bray, Darcie na Edward kama wenyeviti wa bodi.

Wengi wanaooshea kidole uwepo wa sauti nyingi hasa za watoto hawa kwenye maamuzi ya nini kifanyike na nini kisifanyike. Mambo yaweje na yaendeshwaje kwenye klabu. Ingawa kwenye eneo la timu, Meneja wa timu ambaye sasa ni Ten Hag, anakuwa na mamlaka ya moja kwa moja, lakini maamuzi yake ni kwa baraka za watu wajuu.

Pengine yanayoendelea nyuma ya pazia yanawaibua baadhi ya wachezaji ama benchi la ufundi waliowahi kuitumikia klabu hiyo. Pengine ukubwa wa Ronaldo umeleta mjadala mkubwa wa yanayoendelea nyuma ya pazia, lakini wapo waliowahi kuinyooshea kidole United

Jose Mourinho - 'Muda utaongea'

Mourinho (katikati) akiwa na Pogba (wa pili kulia) na Zlatan (kushoto) wanaojiandaa kuingia uwanjani katika moja ya michezo ya United.

Mreno huyu aliifundisha United kuanzia Mei 2016 mpaka December, 2018 alipotimuliwa akiwa katikati ya msimu wake wa tatu United. Baada ya kuondolewa alisema mambo hayako sawa ndani ya United na ‘muda utaongea’.

Alikuja kuyarudia maneno hayo katika mahojiano yake ya Mei 2019, aliyofanya na geziti la Ufaransa la L’Equipe, ikiwa ni miezi mitano baada ya kuondoka Old Trafford.

"Naendelea kusema na kufikiri na nina hisia, lakini umeongea," alisema Mourinho. "Matatizo yanaendelea." Alikuwa akirejea matokeo yasiyoridhisha ya timu hiyo.

Kauli zake zinatafsirika kwamba kwa namna mambo yanavyokwenda, ndivyo klabu hiyo itakavyochelewa kupata matokeo uwanjani.

Masuala hayo mapana yanazunguka kwenye - "wachezaji, taasisi na malengo", kwa mujibu wa Mourinho.

Paul Pogba - Nilipoteza muda Old Trafford

Wakati Paul Pogba anarejea Old Trafford mwaka 2016, lilikuwa tukio kubwa lililopongezwa Manchester United ikitaka kurekebisha makosa ya Sir Alex Ferguson aliyemruhusu kuondoaka awali mwaka 2012.

Lakini haikuonekana hivyo licha ya kuitumikia klabu hiyo kwa misimu 6 kabla ya kuachana nao msimu huu. Alivyoondoka na yeye hakuzungumzia vizuri maisha yake Old Trafford.

Katika mahojiano yake hivi karibuni Mfaransa huyo alisema ni kama alipoteza muda kuwepo Manchester United.

Zlatan - Ina mtazamo wa klabu 'ndogo'

Zlatan Ibrahimovic ni miongoni mwa wanasoka wachache wanaosimamia wanachokiamini. Hapepesi macho. Ana kauli nyingi ‘tata’ na anafahamika kwa kuzungumza anachodhani kiko sawa kwake bila woga.

Licha ya kuichezea kwa misimu miwili ya 2016/2017 na 2017/2018 naye hakuwa nyuma kusema kuhusu Manchester United.

Alidaiwa kuikosoa vikali namna ilivyomruhusu Wayne Ronney kuondoka baada ya miaka 13 ya kuitumikia kwa Mafanikio United, kama vile hakuwahi kuwepo.

Alidaiwa kusema kuwa na klabu hiyo ina mtazamo wa ‘klabu ndogo’ kwa namna ilivyoshughulikia suala la Rooney kuondoka kujiunga na Everton.

Zlatan aliichezea United michezo 53 na kati ya mwaka 2016-2018 na kutwaa Europa League na kombe la ligi mwaka 2017 akiwa na mfungaji bora wa muda wote wa United, Rooney.

Manchester yenyewe inasemaje?

Mara nyingi klabu hiyo imejinasibu kuendeshwa kwa misingi yake. Tangu za Glazier mpaka sasa watoto wake, hoja za kuendeshwa kizamani haipewi nafasi.

Hata alichokisema Ronaldo, Klabu hiyo ilitoa taarifa kwamba inasubiri kupata taarifa kamili kabla ya kujibu.

Inaonekana yapo mengi yanayoendelea nyuma ya pazia, na pengine baada ya mahojiano ya Ronaldo na Morgan kuweka hadharani yote wiki hii, yatabainika mengi.

'Sidhani mchezaji aina ya Ronaldo kwa ukubwa wake na jina lakje, akatoka tu na kuisingizia United, kuna kitu ndani', anasema Raphael Magoha, mfuatiliaji wa soka la kimataifa.

Wakati tukiitarajia pia taarifa rasmi ya United baada ya hapo, angalau itakua hatua muhimu ya kubainisha yanayoendelea nnyuma ya pazia na muelekeo wa Klabu hiyo.