Mataifa ya EAC kwa pamoja kuwa mwenyeji wa AFCON 2027 - Moses Kuria

Nchi za EAC zitashiriki kwa pamoja kuwa mwenyeji wa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka wa 2027 - Kuria.

Muhtasari

• Kuria alisema hayo wakati wa kushuhudia mechi ya kombe la dunia kufuzu hatua ya 16 bora kati ya Uingereza na Wales.

Mawaziri Ababu na Moses Kuria wakiwa na kamishna mkuu wa Uingereza nchini
Mawaziri Ababu na Moses Kuria wakiwa na kamishna mkuu wa Uingereza nchini
Image: Twitter

Waziri wa viwanda, uwekezaji na biashara Moses Kuria ametangaza kuwa mpango upo wa mataifa ya ukanda wa Afrika Mashariki kutuma ombi la kuandaa mashindano ya ubingwa wa bara Afrika AFCON mwaka 2027.

Kuria aliandika dhibitisho hili kupitia ukurasa wake wa Twitter baada ya kuhudhuria mechi ya mashindano ya kombe la dunia nchini Qatar Jumanne akiwa na waziri mwenzake kutoka wizara ya vijana na michezo, Ababu Namwamba.

“Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda, Burundi, DRC, Ethiopia na Sudan Kusini zitashiriki kwa pamoja kuwa mwenyeji wa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka wa 2027. Usiku wa kuamkia leo tumepokea vidokezo muhimu kutoka kwa Kamishna Mkuu wa Uingereza tukifuatilia Mechi ya England na Wales WC,” Kuria alisema.

Kuria anasema hilo wakati kumekuwa na gumzo pevu mitandaoni kuhusu umuhimu wa mataifa yote ya Afrika yote kupewa nafasi ya kuandaa kombe la dunia japo mara moja kila baada ya miaka miwili.

Taifa la Cameroon ndilo la hivi punde kuwa mwenyeji wa mashindano hayo ambayo hufanyika kila baada ya miaka miwili. Katika fainali za mapema mwaka huu, taifa la Senegal liliibuka washindi baada ya kuilemea Misri katika mikwaju ya Penalti.

Wengi wanaamini hilo linawezekana huku wengine pia wakisema kuwa matamshi ya Kuria ni kama matumaini hewa tu kwani ukanda wa Afrika Mashariki hauna uwezo wa kuandaa mashindano hayo kwani hata debi za humu cnhini ni balaa.

“Waziri, Kenya ipi? Ni ile ile ambayo haiwezi kushikilia "Mashemeji Derby" tu na "First Lady's Marathon" siku moja? Michezo bado ni "mchezo" nchini Kenya, si ajabu ninyi nyote mna marais wa shirikisho la michezo fisadi wanaowaingiza vijana wa Kenya wenye vipaji kwenye vishawishi,” Francis  Ngira alisema.