Pele azungumza kufuatia ripoti kwamba amewekwa chini ya uangalizi wa mwisho wa maisha

Hospitali ya Sao Paulo ilisema "bado anaendelea na matibabu na bado yuko sawa".

Muhtasari

•Kumekuwa na tetesi kwamba alikuwa anaanza huduma ya mwisho wa maisha baada ya mwili wake kukataa tiba ya Chemotherapy.

•Alikuwa na uvimbe uliotolewa kwenye koloni lake mnamo Septemba 2021.

Gwiji wa soka wa Brazil Pele
Image: BBC

Gwiji wa kandanda wa Brazil Pele ameweka wazi kuwa "yuko imara na matumaini makubwa" huku akiendelea na matibabu katika hospitali ya Sao Paulo, nchini Brazil.

Haya ni baada ya ripoti nyingi kwamba alikuwa anaanza huduma ya mwisho wa maisha baada ya mwili wake kukataa tiba ya Chemotherapy.Pele amekuwa akipokea matibabu maalum tangu alipogunduliwa na saratani ya matumbo mwaka jana.

Katika taarifa yake ya Jumamosi, alisema jumbe za kumfariji pamoja na kutazama timu ya Brazil kwenye Kombe la Dunia zimempa nguvu.

"Marafiki zangu, ninataka kila mtu awe na utulivu na matumaini," alisema katika kupitia Instagram.

"Niko imara, nikiwa na matumaini makubwa na ninaendelea na matibabu yangu kama kawaida, nataka kuwashukuru timu nzima ya madaktari na wauguzi kwa huduma zote nilizopata.

"Nina imani nyingi kwa Mungu na kila ujumbe wa upendo ninaopokea kutoka kwenu ulimwenguni kote hunifanya nijae nguvu. Na kuitazama Brazil katika Kombe la Dunia pia!

"Asanteni sana kwa kila kitu.

Hapo awali hospitali ya Sao Paulo ilisema "bado anaendelea na matibabu na bado yuko sawa".

Mshindi huyo wa Kombe la Dunia mara tatu, 82 amekuwa hospitalini tangu Jumanne. Siku ya Alhamisi usiku alisema ilikuwa ni "ziara ya kawaida ya kila mwezi".

Alikuwa na uvimbe uliotolewa kwenye koloni lake mnamo Septemba 2021.

Taarifa kutoka kwa Hospitali ya Israelta Albert Einstein siku ya Jumamosi ilisema Pele "alikuwa na mwitikio mzuri wa matibabu ya maambukizo ya kupumua". Iliongeza kuwa alikuwa akifanyiwa utathmini upya wa matibabu ya chemotherapy.

Mshambulizi huyo wa zamani aligundulika kuwa na maambukizo ya kupumua. Ijumaa hospitali ilisema alikuwa katika hali nzuri.

Siku ya Jumamosi, taarifa hiyo mpya ilisema hali yake haijazidi kuwa mbaya katika saa 24 zilizopita.

Jumbe za kumfariji gwiji huyo wa soka zimeendelea kumiminika kutoka kote ulimwenguni