Kutambulishwa kwa Ronaldo Al Nassr kulifuatiliwa na watu 3Bn, fainali za Qatar zilifuatiliwa na 2Bn

Kutambulishwa kwa Ronaldo kulikuwa na watu bilioni 3 kote duniani, huku waliofuatilia kombe la dunia wakiwa bilioni 2.

Muhtasari

• Inaarifiwa watu bilioni 3 walifuatilia kutambulishwa kwa Ronaldo kama mchezaji wa Al Nassr.

• Watu waliofuatilia fainali za kombe la dunia walitajwa kuwa bilioni 2 tu.

Al Nassr yazuiliwa kumchezesha Ronaldo kufuatia kumshambulia shabiki wa Everton.
Al Nassr yazuiliwa kumchezesha Ronaldo kufuatia kumshambulia shabiki wa Everton.
Image: Instagram

Sasa imebainika kuwa hafla ya utambulisho wa mchezaji wa kimataifa wa Ureno Christiano Ronaldo katika timu ya Al Nassr mnamo Jumatatu Jamanne Janauri 3 ilikuwa hafla ya kispoti ambayo ilipata ufuatiliaji mkubwa mitandaoni.

Hafla ya kutambulishwa kwake kama mchezaji rasmi wa Al Nassr ilifuatiliwa na watu wengi zaidi kupita hata idadi ya watu ambao walifuatilia fainali za kombe la dunia nchini Qatar iliyohusisha timu za Argentina na Ufaransa.

Kulingana na Jarida la OJB Sport, hafla ya kutambulishwa kwa Ronaldo mbele ya mashabiki wa timu ya Al Nassr inayoshiriki ligi ya Saudi Arabia ilifuatiliwa na watu bilioni 3 kote duniani kupitia chaneli 40 tofauti.

Idadi hiyo imetajwa kuzidi ile ya watu waliofuatilia fainali za kombe la dunia ambayo iikuwa ni watu bilioni 2 kote duniani.

Cristiano Ronaldo, alitambulishwa kama fowadi wa Al-Nassr kwenye uwanja wa Mrsool Park huko Riyadh, Saudi Arabia.

Ronaldo, ambaye ana mataji matano ya Ligi ya Mabingwa kwa jina lake, alisaini kwa takriban euro milioni 200 hadi Juni 2025 muda mfupi baada ya kutengana kwake na Manchester United.

Mshindi huyo wa tuzo ya Ballon d’Or mara tano alidai kuwa kazi yake Ulaya imekamilika na amehalalisha uhamisho wake wa pesa nyingi kwenda Saudi Arabia kwa kudai kuwa amesaini ‘mkataba wa kipekee kwa kuwa yeye ni mchezaji wa kipekee’.

"Huko Ulaya kazi yangu imekamilika… Nilikuwa na ofa nyingi Ulaya, nyingi huko Brazil, Australia, Marekani, hata Ureno," aliongeza. "Vilabu vingi vilijaribu kunisajili lakini nilitoa neno langu kwa klabu hii."

"Sio mwisho wa kazi yangu kuja Saudi Arabia. Hii ndiyo sababu ninabadilika na, kusema kweli, sina wasiwasi na kile watu wanasema,” Ronaldo alisema.

Mchezaji huyo alikuwa anatarajiwa kucheza mechi yake ya kwanza kama fowadi wa Al Nassr usiku wa Alhamisi lakini hilo halikuwezekana kutokana na marufuku ya mechi mbili ambayo alipatiwa na FA ya uingereza baada ya kupasua simu ya shabiki wa Everton mapema mwezi Novemba mwaka jana.