Kocha ajaribu kutoroka baada ya kushindwa, mwenzake amfuata mbio na kulazimisha salamu (Video)

Juventus walinyukwa mabao 5-1 na Napoli na kocha wa Juve alijaribu kutoroka lakini yule wa Napoli akamfuata na kulazimisha kusalimiwa.

Muhtasari

• Napoli wako kileleni mwa jedwali kwa alama 10 zaidi ya AC Milan ambao wanashikilia nafasi ya pili na mechi moja mkononi.

Usiku wa Ijumaa ligi kuu ya Serie A nchini Italia ilikuwa inaendelea na viongozi wa jedwali Napoli walikuwa wanajuana na mibabe mabingwa mara 36 wa taji hilo, Juventus.

Mechi hiyo ilikuwa inafanyika katika uwanja wa nyumbani wa Napoli, uwanja ambao miaka miwili iliyopita waliubadilisha jina na kuuita Diego Maradona, mchezaji ambaye aliwezesha Napoli kushinda taji la kipekee la Seria A miaka zaidi ya 30 iliyopita mpaka sasa.

Mechi hiyo ilimalizika kwa Juventus kupokezwa kibano cha mabao 5 kwa moja na ilipokamilika kioja cha kuchekesha kilishuhudiwa wakati kocha Massimilliano Allegri wa Juventus alijaribu kutoroka uwanjani kwa aibu kufuatia timu yake kutitigwa bila huruma na viongozi wa jedwali.

Lakini mwenzake wa Napoli Luciano Spalletti hakumuacha aondoke uwanjani hivi hivi kwani alionekana akimkimbilia kwa kasi akijaribu kupata mkono wake wa salamu.

Katika video ambayo imesambazwa vikali Twitter, Allegri aliharakisha kwa kasi nje ya uwanja huku kwa upande mwingine Spalletti akikimbia kando na kusukumana na watu akijaribu kumwahi Allegri ili apate mkono wake.

Kweli, alifanikiwa alipomfikia hatua chache kutoka kuingia ndani ya taneli ya kutoka nje ya uwanja.Allegri kwa aibu alimsalimia Spalletti kabla ya kufululiza nje ya uwanja akiangalia chini ili kamera zisiweze kunasa hisia usoni mwake.

Baada ya ushindi huo, Napoli sasa wamefungua pengo la alama 10 kileleni mwa jedwali na mchezaji wao Victor Osiemhen akiendeleza ubabe wake kwa kufunga mabao mawili katika mechi hiyo na kutoa asisti moja.