Wanabunduki wanasa saini ya Leandro Trossard baada ya kutofautiana na Brighton

Trossard sasa atavalia jazi nambari 19.

Muhtasari

•Trossard sasa atavalia jazi nambari 19 baada ya kukamilisha uhamisho kutoka Brighton na kutia saini mkataba wa miaka mitatu unusu na wanabunduki. 

•Uhusiano wake na Brighton ulisambaratika mapema mwezi huu kufuatia mzozo baina yake na kocha Roberto De Zerbi.

Leandro Trossard amejiunga na Arsenal kutoka Brighton.
Image: HISANI

Klabu ya Arsenal imeng'ata saini ya mshambulizi matata wa Ubelgiji Leandro Trossard.

Trossard sasa atavalia jazi nambari 19 baada ya kukamilisha uhamisho kutoka Brighton na kutia saini mkataba wa miaka mitatu unusu na wanabunduki. 

Uhamisho huo ambao ulikamilika siku ya Ijumaa unadaiwa kuigharimu Arsenal pauni milioni 21 (Sh3.2b) pamoja na marupurupu ya hadi pauni milioni 5.

"Stakabadhi zote zimewasilishwa na tunatumai Leandro atastahili kuchaguliwa kwa mechi yetu dhidi ya Manchester United siku ya Jumapili," taarifa rasmi ya Arsenal kuhusu usajili wa mshambulizi huyo ilisoma.

Mshambulizi huyo mwenye umri wa miaka 28 pia alishiriki katika mazoezi ya Wanabunduki ya Ijumaa huku viongozi hao wa Ligi Kuu wakijiandaa kwa mechi yao kubwa dhidi ya Mashetani Wekundu siku ya Jumapili.

Akizungumza baada ya kusaini mkataba wake, Trossard alisema kuwa alifurahi sana kusajiliwa katika klabu hiyo ya London.

"Nimefurahi sana kuanza. Bila shaka hii ni klabu kubwa, niko tayari kuwaonyesha mashabiki kile ninachoweza kufanya," alisema.

Meneja Mikel Arteta alidokeza kwamba wamekuwa wakimfuatilia mshambulizi huyo kwa muda mrefu na kudai atakuwa nyongeza muhimu.

“Tuna furaha sana kuwa naye. Ni mchezaji ambaye tumemfuata kwa muda sasa... tulikuwa na hitaji la kuwa na mchezaji katika mstari wa mbele ambaye ana uwezo wa kucheza katika nafasi tofauti." alisema Arteta.

Trossard amejiunga na Arsenal baada ya kuchezea Brighton kwa takriban miaka mitatu. 

Mshambuliaji huyo alijiunga na Seagulls mwezi Juni  mwaka wa 2019 kabla ya uhusiano wake na klabu hiyo kusambaratika mwishoni mwa mwaka jana kufuatia mzozo baina yake na kocha mkuu Roberto De Zerbi.

Trossard amekuwa akipigania kuondoka Brighton kwani alihisi "amefedheheshwa" na  De Zerbi baada ya kuachwa nje katika mechi za majuzi za Brighton.Kocha huyo kwa upande wake alisema hakupendezwa na mtazamo wa Trossard katika mazoezi.