Mbunge George Aladwa alipa usafiri wa Vihiga Bullets baada ya kukwama Nairobi

Aladwa alitoa elfu 35 kusimamia usafiri wao kurudi Vihiga.

Muhtasari

• Mechi kati ya Bullets na AFC Leopards iliisha kwa kufungwa bao moja kapa na Ingwe.

• Kocha alisema wachezaji wake waliingia uwanjani wakiwa matumbo tupu bila kula kitu tangu waliposafiri kutoka Vihiga.

Mbunge Aladwa aikwamua Bullets
Mbunge Aladwa aikwamua Bullets
Image: Facebook

Mbunge wa Makadara kaunti ya Nairobi George Aladwa ametoa msaada wa fedha za usafiri kwa timu ya Vihiga Bullets iliyokuwa imekwama Nairobi baada ya kushiriki mechi ya ugenini dhidi ya AFC Leopards.

Mechi hiyo ya ligi kuu ya FKF iliisha kwa AFC kuwalaza Vihiga bao moja kapa na baadae walishindwa kusafiri kurudi zao Vihiga kupelekea kocha mkuu George Owoko kuomba msaada kwa wasamaria wema kuwawezesha kusafiri kwenda Magharibi.

Taarifa hizo zilifichuliwa na mtangazaji wa Radio Jambo Fred Arocho kupitia mtandao wake wa Facebook na Aladwa baada ya kuona ujumbe huo, alimfikia kocha Owoko na kutoa msaada wa shilingi elfu 35 ili kuwawezesha kusafiri.

“Nataka kumshukuru Mhe George Aladwa kwa kuja kutusaidia. Sasa tuko tayari kusafiri kwenda nyumbani. Ombi letu pia lilimgusa Bw George Achar ambaye ni mfanyabiashara nchini Marekani. Kwa niaba ya timu, ninamshukuru. Mungu ambariki Aladwa na Achar kwa kutufanyia wema huu,” kocha Owoko alisema.

"Tulishindwa na pesa zilizokusanywa sasa zitashughulikia milo yetu tukiwa njiani kurudi nyumbani, mafuta kati ya vifaa vingine. Tunashukuru kwa kitendo hiki cha aina yake,” aliongeza.

Kocha huyo alisema kuwa Ili kuenzi mchezo huo, Bullets ilichangisha pesa kutoka kwa michango kutoka kwa bodaboda, mama Mboga, wafanyabiashara na jamii ya eneo la Mbale, Kaunti ya Vihiga.

Wachezaji hao walijitokeza kwa ajili ya mechi dhidi ya Leopards wakiwa matumbo tupu tangu walipokula kiamsha kinywa asubuhi pekee.