Mwanachama wa Arsenal ateuliwa kuchunguza Man City kwa ukiukaji wa kanuni

Endapo ManCity watapatikana na hatia, huenda wakapokonywa pointi 15 au hata kufukuzwa kutoka kwa ligi kuu ya Premia.

Muhtasari

• Manchester City sasa wanakabiliwa na uchunguzi mkali ambao utatoa hatma kama watachukuliwa hatua au wataachiwa huru.

• Imebainika mmoja wa majaji walioteuliwa kuendesah uchunguzi huo ni shabiki na mwanachama wa Arsenal wa muda mrefu.

Barrister Murray, jaji wa Arsenal atakayeichunguza Mancity.
Barrister Murray, jaji wa Arsenal atakayeichunguza Mancity.
Image: Twitter

Baada ya klabu ya Manchester City kupatikana na tuhuma za kukiuka kanuni za usajili kwa miaka kadhaa, kamati maalum imeteuliwa ili kuzamia uchunguzi huo ambao utatoa hatma iwapo timu hiyo inakabidhiwa adhabu au itanusurika.

Sasa imebainika kuwa mmoja wa majaji ambao wameteuliwa katika bodi ya uchunguzi huo dhidi ya City ni shabiki wa muda mrefu wa timu ya Arsenal – wapinzani wakali wa City msimu huu kuelekea ubingwa wa ligi kuu ya Premia.

Majarida ya Uingereza yanaripoti kuwa Barrister Murray Rosen KC ameteuliwa kuwa mwenyekiti wa tume huru inayochunguza Mancity. Pia atakabidhiwa kuwateua wajumbe wengine wa jopo ambao wanaweza kuwapata City na hatia ya kupelekea kukatwa pointi.

Hata hivyo, wakati wanachama wa Wakili wa Mfalme wanachukuliwa kuwa na uzoefu sana kuathiriwa na matukio na sauti za nje, Rosen ni shabiki wa Arsenal mwenye shauku.

"Yeye ni muumini mkubwa wa haki na nguvu na faida za michezo na anathamini sana nyanja zake za kijamii, kisiasa na kifedha," wasifu wa Rosen kwenye vyumba 4 vya New Square uliandika kulingana na Daily Star. "Ameshiriki katika mchezo maisha yake yote, ni mwanachama wa MCC na Arsenal FC, na bado anacheza tenisi halisi na ping pong mara kwa mara.”

Kikosi cha Pep Guardiola kilishindwa kufurukuta mbele ya The Gunners katika mbio za ubingwa baada ya kufungwa 1-0 na Tottenham Hotspur siku ya Jumapili. City wako pointi tano nyuma ya kikosi cha Mikel Arteta, lakini pengo hilo litaongezeka hadi pointi nane ikiwa Arsenal itashinda mchezo wao wa mkononi.

Hata hivyo, matatizo ya City uwanjani yanaweza kuwa mabaya hivi karibuni kwani Ligi ya Premia hivi majuzi ilitangaza kuwa klabu hiyo imeshtakiwa kwa ukiukaji wa zaidi ya 100 wa kanuni za kifedha. Na mtu aliyepewa dhamana ya kusimamia tume huru ya masuala ya City ni mfuasi wa Arsenal.