Refa aliyeruhusu bao la kuotea la Brentford dhidi ya Arsenal aacha kazi

Lee Mason aliondoka PGMOL kwa maelewano siku ya Ijumaa.

Muhtasari

•Lee Mason aliruhusu bao la mshambulizi Ivan Toney baada ya kukosa kuchora mstari kubaini kama kulikuwa na mchezaji yeyote wa klabu ya Brentford ambaye alikuwa ameotea.

• PGMOL ilikiri kuwa hitilafu ya kibinadamu ilitokea kwenye mechi hiyo na hata ikaomba msamaha kufuatia hilo

hatasimamia tena mechi ya EPL
Refa Lee Mason hatasimamia tena mechi ya EPL
Image: HISANI

Refa aliyeruhusu bao la kuotea la Brentford lililowafanya watoke sare na Arsenal wikendi iliyopita hatasimamia tena mechi za EPL.

Refa Lee Mason aliondoka Professional Game Match Officials Limited  (PGMOL) kwa maelewano siku ya Ijumaa kufuatia kosa lake la kusimamia mechi lililosababisha wanabunduki kudondosha pointi mbili muhimu katika mbio zao za kuwania taji la EPL ambalo wamekuwa wakisubiri kwa karibu miongo miwili.

Jumamosi iliyopita, Lee Mason aliruhusu bao la mshambulizi Ivan Toney baada ya kukosa kuchora mstari kubaini kama kulikuwa na mchezaji yeyote wa klabu ya Brentford ambaye alikuwa ameotea.

Mchuano huo uliishia sare ya 1-1 na kusababisha ghadhabu kubwa miongoni mwa mashabiki wa Arsenal ambao walikuwa na uhakika kwamba kuna mchezaji mmoja wa timu hiyo nyingine aliyekuwa ameotea.

Baadae, PGMOL ilikiri kuwa hitilafu ya kibinadamu ilitokea kwenye mechi hiyo na hata ikaomba msamaha kufuatia hilo.

"Tunakubali makosa yalifanywa. Hata hivyo, tunatiwa moyo na jinsi maafisa wetu walivyoitikia na tuna imani kwamba wataendeleza mafunzo," Bodi hiyo ya kusimamia marefa wa Ligi Kuu ya Uingereza ilisema.

Meneja wa Arsenal Mikel Arteta alikasirishwa sana na makosa hayo ambayo yanaweza kuwa ghali sana katika mbio zao za kuwashinda Manchester City na kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza.

Siku ya Jumanne, Arteta alikubali msamaha wa PGMOL kwa kusita huku akisema angeridhika iwapo wangerejeshewa pointi mbili walizopoteza.

"Nashukuru msamaha huo wa dhati, lakini haiondoi ukweli kwamba tuna pointi mbili chache zaidi. Kila mtu hufanya makosa lakini hiyo ilikuwa kitu kingine. Sikulikubali, klabu pia haikulikubali," aliambia wanahabari.

Siku nne baadae, Wanabunduki waliendelea kupoteza mchuano dhidi ya mabingwa watetezi Manchester City na kushuka kutoka kileleni mwa jedwali hadi nafasi ya pili baada ya kuongoza kwa muda mrefu.