CR7 ashinda tuzo yake ya kwanza katika ligi ya Saudia, miezi 2 tu tangu kwenda Al Nassr

Mchezaji huyo alifurahia tuzo hiyo na kusema kwamba ndio ya kwanza katika nyingi ambazo anazitarajia kushinda Uarabuni.

Muhtasari

• Tangu ajiunge na klabu yake mpya, Ronaldo amefunga mabao manane na kutoa pasi mbili za mabao.

• Ronaldo alifunga bao lake la kwanza la Al Nassr katika sare yao ya 2-2 dhidi ya Al Fateh mnamo Februari 3

Ronaldo akiwa na tuzo ya Roshn kama mchezaji bora wa Februari.
Ronaldo akiwa na tuzo ya Roshn kama mchezaji bora wa Februari.
Image: Facebook

Staa wa soka kutoka Ureno Christiano Ronaldo ameshinda tuzo yake ya kwanza kama mchezaji wa Al Nassr katika ligi kuu nchini Saudi Arabia, miezi miwili tu baada ya kuhamia katika taifa hilo la Uarabuni.

Ronaldo alituzwa kama mchezaji bora wa mwezi Februari maarufu kwa jina Roshn na alionesha furaha yake akisema kwamba ndio mwanzo anafungua rafu ya tuzo zake katika ligi hiyo mpya kwake.

“Nina furaha kushinda tuzo ya Mchezaji Bora wa mwezi wa Februari kwa Ligi ya Roshn Saudi. Natumai ya kwanza kati ya nyingi! Najivunia kuwa sehemu ya timu hii Al-Nassr,” Ronaldo alisema kweney mitandao ya kijamii.

CR7 aliwasili Al Nassr baada ya klabu hiyo ya Saudia kufanikiwa kumsajili kwa mkataba wa hali ya juu mwezi Januari. Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ureno amepata mdundo wake haraka katika Ligi ya Saudi Pro, akicheza jukumu muhimu katika safu ya ushambuliaji ya timu yake.

Tangu ajiunge na klabu yake mpya, Ronaldo amefunga mabao manane na kutoa pasi mbili za mabao. Maonyesho ya CR7 yamesaidia Al Nassr kudumisha nafasi yao kileleni mwa jedwali la Saudi Pro League.

Ronaldo alifunga bao lake la kwanza la Al Nassr katika sare yao ya 2-2 dhidi ya Al Fateh mnamo Februari 3. Kisha akafunga mabao yote manne ya timu yake dhidi ya Al Wehda wiki moja baadaye.

CR7 alikamilisha maonyesho yake mazuri mwezi Februari kwa kufunga hat-trick katika ushindi wa 3-0 wa Al Nassr dhidi ya Damac wiki iliyopita. Ushindi huo uliwaweka Ronaldo na wenzake kileleni mwa jedwali la Saudi Pro League, pointi mbili juu ya Al Ittihad.