Mchezaji wa zamani wa Gor Mahia kuuza basi la timu hiyo kujilipa deni lake

Inaarifiwa kwamba malimbikizi yake ambayo Gor haijawahi kumlipa ni Zaidi ya shilingi milioni moja.

Muhtasari

• Beki huyo alifanikiwa kuishtaki Gor Mahia katika Mahakama za Milimani na sasa basi hilo la timu ya Gor Mahia limewekwa sokoni.

Mchezaji Wellintone Ochieng kuuza basi la Gor kujilipa
Mchezaji Wellintone Ochieng kuuza basi la Gor kujilipa
Image: Facebook

Mwanasoka wa Kenya Wellington Ochieng amewasilisha ombi kwa mahakama ya kibiashara kupiga mnada basi la Gor Mahia ili kurejesha malimbikizo ya mishahara anayodaiwa na klabu hiyo ya soka.

Beki huyo alifanikiwa kuishtaki Gor Mahia katika Mahakama za Milimani na sasa basi hilo la timu ya Gor Mahia limewekwa sokoni, kulingana na tangazo la kupigwa mnada lililoonekana kwenye jarida moja la humu nchini.

Kampuni ya kupiga mali mnada ya Vintage ilipokezwa zabuni hiyo na kuweka tangazo la kibiashara kwenye jarida moja wakisema kwamba kesi hiyo ya Ochieng dhidi ya Gor Mahia ilikamilika katika mahakama ya Milimani.

“Chini ya maagizo tuliyopokea kutoka kwa mahakama ya Milimani, tunatangaza kuuza gari hili ambalo limetajwa hapa ambalo limeshikiliwa katika karakana ya Leakey. Gari hili litauzwa Machi 15 mwaka 2023 saa nne na nusu asubuhi katika ofisi zetu,” sehemu ya tangazo hilo ilisoma.

Klabu hiyo kwa sasa inatumikia adhabu iliyowekewa na Fifa kwa kushindwa kuwalipa wachezaji wake kwa wakati na kutoruhusiwa kusajili wachezaji wapya.

 

Ochieng, 27, aliiwakilisha Gor Mahia kwa miaka miwili kati ya 2016 na 2018 na inaarifiwa kwamba malimbikizi yake ambayo Gor haijawahi kumlipa ni Zaidi ya shilingi milioni moja.

Alianza maisha yake ya ujana mjini Kisumu, akitokea katika Chama cha Soka cha Vijana cha Kisumu cha Amani FC na Urusi FC.

Kisha akawa nahodha wa Agrochemicals FC katika ligi ya daraja la tatu kabla ya kujiunga na Muhoroni Youth kabla ya matokeo yake ya kuvutia uwanjani kuvutia Gor.

Beki wa kulia wa pembeni pia amewakilisha timu ya taifa ya kandanda ya Kenya.

Baada ya kuondoka Gor, Wellington alijiunga na Tusker ambapo pia baada ya miezi michache alikatiza kandarasi yake na sasa yuko huru ila anasisitiza bado hajastaafu kutoka kwa soka.