Ten Haag aeleza kwa nini imekuwa ngumu kwa Man United kushindana na Arsenal

Kocha huyo alibainisha kuwa Wanabunduki hawajakumbana na matatizo kama yao sana.

Muhtasari

•Ten Haag alibainisha kuwa msimu huu amekwenda kwenye mechi moja tu wachezaji wake wote wakiwa tayari kuhusishwa.

•Kocha huyo wa zamani wa Ajax alilalamika kuwa sababu mbalimbali zimewazuia wachezaji tofauti katika baadhi ya mechi.

Erik ten Hag
Erik ten Hag
Image: EURO SPORT

Meneja Mkuu wa Manchester United, Erik Ten Haag amelalamika kwamba amelazimika kushiriki michuano mingi ya Ligi Kuu ya msimu huu wa 2022/23  bila angalau mmoja wa wachezaji wakuu wa klabu hiyo.

Wakati akizungumza na Waandishi wa Habari, kocha huyo Mholanzi mwenye umri wa miaka 53 alibainisha kuwa msimu huu amekwenda kwenye mechi moja tu wachezaji wake wote wakiwa tayari kuhusishwa.

"Ni katika mechi moja tu ambapo nilisema, sawa, sasa ninaweza kuchagua timu yangu kwa mbinu ya kiufundi ambayo ni nzuri. Hiyo ilikuwa dhidi ya Man City. Ilikuwa mara ya pekee msimu huu," Kocha huyo alisema.

Kocha huyo wa zamani wa Ajax alilalamika kuwa sababu mbalimbali zimewazuia wachezaji tofauti katika baadhi ya mechi.

"Katika kila mchuano unapata kuna mchezaji mmoja ambaye amesimamishwa kucheza, mchezaji mmoja amejeruhiwa au ni mgonjwa. Tunapaswa kukabiliana nayo vyema, lakini bila shaka unakuwa na matumaini," alisema.

Ten Haag alibainisha kuwa mmoja wa wapinzani wao wakuu, Arsenal, ambao wanaongoza ligi kwa sasa, hawajakumbana na matatizo kama hayo sana. Alidokeza kuwa hiyo ndiyo sababu ya klabu hiyo ya London kung'aa.

"Ukiangalia, Arsenal karibu kila wakati, wachezaji wote wanapatikana," alisema.

Mashetani Wekundu kwa sasa wako kwenye nafasi ya tatu ya jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza wakiwa na pointi 50 baada ya kucheza mechi 26 kati ya 38 za EPL 2022/23.

Wanabunduki kwa upande mwingine wanaongoza jedwali wakiwa na pointi 66 kati ya mechi 27 za Ligi Kuu ambazo wamecheza msimu huu. Wanafuatwa na Manchester City ambao wamezoa pointi 60 kutoka kwa mechi 27 walizocheza.