"Mimi ni mtu bora sasa" Chritiano Ronaldo akiri kuwa na taaluma mbaya katika Man U

Ronaldo amesema kuwa yeye sasa ni mtu bora baada ya yeye kuondoka katika Manchester United.

Muhtasari

•Mshambulizi huyo alikiri kwamba alikuwa na kipindi kibaya cha taaluma yake ya soka wakati akiwa katika United.

•Ronaldo alibainisha kuwa taaluma yake ya soka inaendelea vizuri sasa na kusema kuwa kipindi chake katika Man U kilikuwa sehemu ya ukuaji wake.

Amefichua kuwa hana raha katika klabu hiyo ya Premier league.
Mshambulizi wa Manchester United Christiano Ronaldo. Amefichua kuwa hana raha katika klabu hiyo ya Premier league.
Image: GETTY IMAGES

Mshambulizi wa Ureno Christiano Ronaldo amesema kuwa yeye sasa ni mtu bora baada ya yeye kuondoka katika Manchester United.

Ronaldo aliwaaga Mashetani Wekundu mwezi Januari mwaka huu kufuatia mahojiano yake yenye utata na mtangazaji wa Uingereza, Piers Morgan ambapo alifichua mambo ya ndani ya klabu hiyo hadharani.

Akizungumza kwenye mahojiano nchini Ureno, kabla ya mechi zao za kipindi cha mapumziko ya kimataifa, mshambulizi huyo alikiri kwamba alikuwa na kipindi kibaya cha taaluma yake ya soka wakati akiwa katika United.

"Wakati mwingine, lazima upitie mambo mengine ili kuona ni nani aliye upande wako. Sina shida kusema, nilikuwa na kipindi kibaya, lakini hakuna wakati wa majuto," alisema.

Mshambulizi huyo mwenye umri wa miaka 38 alibainisha kuwa taaluma yake ya soka inaendelea vizuri kwa sasa na kusema kuwa kipindi chake kibaya katika Manchester United kilikuwa sehemu ya ukuaji wake.

"Tunapokuwa juu ya mlima, mara nyingi hatuwezi kuona kilicho chini. Sasa, nimejitayarisha zaidi na kujifunza jambo ambalo lilikuwa muhimu, kwa sababu sikuwahi kupitia haya, kama katika miezi michache iliyopita. Sasa mimi ni mtu bora," alisema.

Ronaldo alijiunga na klabu ya Al Nassr mwezi Januari baada ya mkataba wake na Manchester United kutamatishwa. Uhusiano wa mshambulizi huyo na United uliingia dosari baada ya mahojiano yake na Morgan kupeperushwa.

Kwenye mahojiano hayo, mshambulizi huyo aliweka wazi kwamba hakuwa na raha katika klabu hiyo inayoshabikiwa sana.

Christiano alidai kuwa baadhi ya watu katika uongozi wa klabu hiyo akiwemo kocha Erik Ten Hag  wamekuwa wakijaribu kumtimua nje kwa nguvu tangu msimu uliopita, jambo ambalo linamfanya ahisi amesalitiwa.

"Wamekuwa wakijaribu kunitoa, sio kocha tu. Pia watu wengine watatu hivi kwenye klabu. Nilihisi nimesalitiwa," alisema.

Mshambulizi huyo mwenye umri wa miaka 38 alisema alihisi kusalitiwa kwani yeye ni mtu anayepaswa kuheshimiwa na kusikilizwa.

Alipoulizwa kwa nini viongozi wakuu wa klabu walikuwa wakijaribu kumfukuza, mchezaji huyo wa timu ya taifa ya Ureno alijibu: "Kusema kweli, sijui. Sijali. Watu wanapaswa kusikia ukweli. Ndiyo, nahisi kusalitiwa. Baadhi ya watu hawakutaka niwe hapa sio mwaka huu tu, bali mwaka jana pia."

Aidha aliweka wazi kuwa hana heshima yoyote kwa kocha wa United, Erik teg Hag,  kwani pia yeye  hajaonyesha heshima kwake.

"Simheshimu Erik ten Hag kwa sababu haonyeshi heshima kwangu. Ikiwa huniheshimu, sitawahi kukuheshimu," alisema.

Christiano pia aliibua madai kwamba hakujakuwa na mabadiliko yoyote katika klabu ya Manchester United tangu kuondoka kwa aliyekuwa kocha mkuu, Sir Alex Ferguson takriban miaka tisa iliyopita.

"Nilidhani nikirudi ningeona vitu tofauti; teknolojia, miundombinu. Kwa bahati mbaya, tunaona vitu vingi ambavyo nilizoea kuona nikiwa na miaka 21, 22, 23. Ilinishangaza sana," alisema.

Alikosoa uteuzi wa Ralf Rangnick  kama kocha wa muda baada ya kutimuliwa kwa Ole Gunnar Solskjær mwaka jana.