N'Golo Kanté afeli vipimo vya afya katika azma ya kwenda Saudia kutoka Chelsea

Kante, 32, ana historia ya majeraha na alikosa miezi sita ya msimu wa Ligi Kuu ya Chelsea kutokana na tatizo la misuli ya paja.

Muhtasari

• Siku ya Jumanne, klabu hiyo yenye makao yake mjini Jeddah ilimtambulisha rasmi mshindi wa tuzo ya Ballon d'Or ya Ufaransa Karim Benzema.

• Benzema na Kante wako kwenye orodha ya takriban walengwa 10 ambao wamewasiliana na maafisa wa Saudi.

N'golo Kante afeli afya katika azma ya kwenda Saudi Arabia.
N'golo Kante afeli afya katika azma ya kwenda Saudi Arabia.
Image: Facebook

Safari ya kiungo wa kati wa Chelsea, Mfaransa Ngolo Kante kuelekea Saudi Arabia kujiunga na timu ya Al Ittihad huenda italazimika kusubiriwa Zaidi baada ya taarifa za ndani kutoka kwa timu hiyo ya Saudia kufichua kwamba Mfaransa huyo alifeli katika vipimo vya afya.

Kulingana na jarida la AFP, Kante alikuwa amekubali mkataba wa kumweka Al Ittihad hadi mwaka 2026 lakini awamu ya mwisho na ambayo ni muhimu ya vipimo vya matibabu ikifeli.

Kante, 32, ana historia ya majeraha na alikosa miezi sita ya msimu wa Ligi Kuu ya Chelsea kutokana na tatizo la misuli ya paja.

Chanzo cha Al-Ittihad kilisema Kante alitia saini makubaliano ya lazima lakini klabu hiyo inachunguza matokeo ya vipimo vya afya kabla ya kukubaliana mkataba wa mwisho.

Siku ya Jumanne, klabu hiyo yenye makao yake mjini Jeddah ilimtambulisha rasmi mshindi wa tuzo ya Ballon d'Or ya Ufaransa Karim Benzema mwenye umri wa miaka 35 kama mchezaji mkubwa zaidi katika historia yao.

"Kante alisaini makubaliano ya lazima, sio mkataba wa mwisho," chanzo kilinukuliwa na AFP.

"Bado tunapitia matokeo ya uchunguzi wa afya. Ana historia ndefu ya majeraha na tunataka kuwa makini kabla ya kusaini mkataba mkubwa."

Usajili wa Benzema umekuja baada ya supastaa wa Ureno Cristiano Ronaldo kujiunga na Al-Nassr ya Saudi Arabia mwezi Januari kwa mkataba unaodaiwa kuwa wa zaidi ya euro milioni 400.

Benzema na Kante wako kwenye orodha ya takriban walengwa 10 ambao wamewasiliana na maafisa wa Saudi, chanzo kilicho karibu na mazungumzo hayo kiliiambia 'AFP' wiki iliyopita.

Mchezaji wa Argentina Lionel Messi alitangaza siku ya Jumatano kuwa amekataa kandarasi ya juu kabisa huko Saudi Arabia ili ajiunge na Inter Miami ya MLS.