Mo Salah kugura Liverpool kwenda Saudia?- Jurgen Klopp apasua mbarika

Klopp amepuuzilia mbali taarifa za mshambuliaji Mo Salah kujiunga na klabu ya Al Ittihad ya Saudi Arabia.

Muhtasari

•Klopp alidokeza kwamba bado hajapokea au kusikia kuhusu ofa zozote za ununuzi wa staa huyo wa soka kutoka nchi hiyo ya bara Asia.

•"Ikiwa kuna kitu (ofa) kinakuja, ambacho sijui, basi itabidi nifikirie juu yake. Lakini kama kungekuwa na kitu, itakuwa hapana,” alisema.

Image: HISANI

Meneja wa Liverpool Jurgen Klopp amepuuzilia mbali taarifa za mshambuliaji Mo Salah kujiunga na klabu ya Al Ittihad ya Saudi Arabia.

Wakati akizungumza na waandishi wa habari siku ya Ijumaa kabla ya mechi za EPL wikendi hii, Klopp alidokeza kwamba bado hajapokea au kusikia kuhusu ofa zozote za ununuzi wa staa huyo wa soka kutoka nchi hiyo ya bara Asia.

Kocha huyo mwenye umri wa miaka 56 alizidi kuweka wazi kuwa klabu haina nia ya kumuuza nahodha huyo wa timu ya taifa ya Misri.

"Hakuna cha kuzungumza kwa mtazamo wetu. Hatuna ofa, Mo Salah ni mchezaji wa Liverpool. Hakuna kitu hapo, hata kama kingekuwepo, jibu litakuwa hapana," Klopp alisema.

Aliongeza, "Ikiwa kuna kitu (ofa) kinakuja, ambacho sijui, basi itabidi nifikirie juu yake. Lakini kama kungekuwa na kitu, itakuwa hapana.”

Kocha huyo kutoka Ujerumani pia alidokeza kwamba Mo Salah amejitolea kwa asilimia mia moja kuichezea Liverpool na hajatoa shinikizo la kuondoka Anfield.

Mo Salah ndiye mchezaji tajika wa hivi punde kuhusishwa na kuhamia kwenye ligi ya Saudia ambayo tayari imewawinda wachezaji wengi wakubwa.

Miongoni mwa wachezaji bora ambao tayari wamejiunga na ligi ya Saudi Arabia ni pamoja na Christiano Ronaldo (Al Nassr), Neymar Santos Jr (Al Hilal), Karim Benzema (Al-Ittihad), Sadio Mane (Al Nassr), Jodan Henderson (Al- Ettifaq). ), Ng'olo Kante (Al-Ittihad), Roberto Firmino (Al-Ahli), Kalidou Koulibaly (Al-Hilal), Edouard Mendy (Al-Ahli), Riyad Mahrez (Al -Ahli), Fabinho (Al-Ittihad) miongoni mwa wengine.