Kashfa ya kumpiga busu mchezaji yamfuta kazi kocha wa timu ya taifa ya wanawake ya Hispania

Katika taarifa yake, shirikisho la Hispania RFEF halijatoa sababu mahususi za kutimuliwa kwa Vilda.

Muhtasari

•Ushindi wa Hispania ulifunikwa na kashfa ya rais wa shirikisho la soka nchini humo Rubiales kumbusu mshambuliaji Jenni Hermoso.

Image: HISANI

Jorge Vilda, kocha mkuu wa timu ya taifa ya wanawake iliyotwaa hivi majuzi Kombe la Dunia la Wanawake, amefukuzwa kazi kutokana na kashfa inayoendelea ya Luis Rubiales.

Ushindi wa Hispania ulifunikwa na kashfa ya rais wa shirikisho la soka nchini humo Rubiales kumbusu mshambuliaji Jenni Hermoso, jambo ambalo alisema lilikuwa la makubaliano.

Wengi katika benchi la ufundi la Vilda walijiuzulu huku wachezaji 81 wakikataa kuichezea Hispania baada ya tukio hilo. Rubiales amekataa kujiuzulu lakini amesimamishwa kwa muda na Fifa, shirikisho la soka duniani.

Katika taarifa yake, shirikisho la Hispania RFEF halijatoa sababu mahususi za kutimuliwa kwa Vilda.

Hata hivyo, RFEF imekuwa ikichunguza kama inaweza kumtimua Vilda - anayechukuliwa kuwa mshirika wa karibu wa Rubiales - tangu wiki iliyopita.

Alionekana akimpigia makofi Rubiales kwenye mkutano mkuu usio wa kawaida wa RFEF mapema mwezi Agosti - wakati Rubiales alipokuwa akisisitiza mara kwa mara kuwa hatajiuzulu na kusema angempa Vilda mkataba mpya..