Sababu ya Paul Pogba kupatikana na hatia ya matumizi ya dawa haramu yafichuka

Pogba amekiri na kujutia kutoitaarifu klabu kuhusu ununuzi wa virutubisho hivyo na kutoshauriana na madaktari wa klabu.

Muhtasari

•Pogba anaripotiwa kukiri kutumia virutubisho vya lishe bila kujua kuwa vina testosterone ambayo ni dawa iliyopigwa marufuku.

•Pogba aliiambia Juventus kwamba hakujua kuwa kuna testosterone katika virutubisho vya chakula alichotumia

Image: BBC

Kiungo wa kati wa Juventus Paul Pogba anaripotiwa kukiri kutumia virutubisho vya lishe bila kujua kuwa vina testosterone ambayo ni dawa iliyopigwa marufuku.

Jarida la Kimataifa la Habari za Michezo, ESPN linaripoti kwamba kirutubisho cha chakula alichoandikiwa mchezaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa na rafiki yake ambaye ni daktari nchini Marekani kilipelekea kupimo cha dawa haramu na hatari ya kupigwa marufuku kwa muda wa miaka minne.

Pogba kwa sasa anasubiri matokeo ya sampuli B, ambayo yanapaswa kuja kabla ya mwisho wa wiki, lakini yanatarajiwa kuwa sawa ya awali. Huku akisubiri matokeo ya sampuli  B, anahatarisha kupigwa marufuku kwa hadi miaka minne.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 30 inasemekana aliiambia Juventus kwamba hakujua kuwa kuna testosterone katika virutubisho vya chakula alichotumia, kosa ambalo anakiri na kujutia kutoitaarifu klabu kuhusu ununuzi wa bidhaa hiyo na kutoshauriana na madaktari wa klabu hiyo.

Mapema wiki hii, Paul Pogba alipigwa marufuku ya muda kucheza soka kwa kosa la kutumia dawa za kusisimua misuli.

Vipimo viliyofanywa kwa kiungo huyo wa kati  na tume ya kitaifa ya Italia ya kupambana na dawa za kusisimua misuli (Nado) vilionyesha viwango vya testosterone. Testosterone ni homoni ambayo huongeza uvumilivu wa wanariadha.

Pogba alifanyiwa vipimo baada ya klabu yake ya sasa Juventus kushinda 3-0 dhidi ya Udinese mnamo Agosti 20. Mchezaji huyo wa zamani wa Manchester United alikuwa mchezaji wa akiba ambaye hakutumika wakati wa mechi lakini alichaguliwa kwa uchunguzi wa dawa za kulevya baada ya mechi.

Iwapo atapatikana na hatia ya kutumia dawa za kusisimua misuli, anaweza kupigwa marufuku kati ya miaka miwili na minne.

Jumatatu jioni, Juventus ilitoa taarifa kuthibitisha taarifa hizo ikisema kiungo huyo amesimamishwa kwa muda.

"Klabu ya Soka ya Juventus inatangaza kwamba leo, Septemba 11, 2023, mchezaji wa mpira wa miguu Paul Labile Pogba amepokea amri ya tahadhari ya kusimamishwa kutoka kwa Tume ya Kitaifa ya Kupambana na Dawa za Kulevya kufuatia matokeo ya vipimo vilivyofanywa tarehe 20 Agosti, 2023," ilisema taarifa hiyo.

Nado alisema Pogba alikiuka sheria za kupinga matumizi ya dawa za kusisimua misuli walipopata dawa iliyopigwa marufuku "metaboli za testosterone zisizo asilia" na matokeo "yaliendana na asili ya nje ya misombo inayolengwa".