AFL: CAF yatoa ratiba ya mkondo wa kwanza wa fainali kati ya Wydad na Mamelodi Sundowns

Mshindi wa Uzinduzi wa Ligi ya Soka ya Afrika (“AFL”) atapata Tuzo ya Pesa ya dola za Kimarekani milioni 4, sawa na pesa za Kenya shilingi milioni 595.

Muhtasari

• Fainali ya kwanza itachezwa mjini Casablanca nchini Morocco huku ya pili ikichezwa Afrika Kusini.

Kombe la African Football League
Kombe la African Football League
Image: CAF

Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika, CAF, limetangaza tarehe na nyakati za mechi ya Fainali ya mkondo wa kwanza na wa pili wa Ligi ya Soka ya Afrika, AFL, kati ya Wydad Athletic Club ya Morocco na Mamelodi Sundowns kutoka Afrika Kusini.

Wydad AC watakuwa wenyeji wa mkondo wa kwanza wa Fainali inayotarajiwa kuwa ya kusisimua kati ya Vilabu viwili mahiri zaidi barani Afrika Jumapili, 05 Novemba 2023 nchini Morocco katika Uwanja wa Casablanca Stade Mohammed V saa moja jioni kwa saa za huko, CAF walithibitisha kupitia tovuti yao rasmi.

Mechi ya mkondo wa pili itachezwa Pretoria (Tshwane), Afrika Kusini kwenye Uwanja wa Loftus Versfeld Jumapili, 12 Novemba 2023 saa tisa alasiri kwa saa za huko ambapo Mabingwa wa Uzinduzi wa Ligi ya Soka ya Afrika (“AFL”) watakabidhiwa taji.

Ligi ya Soka ya Afrika (“AFL”) ni shindano la CAF lililoanzishwa kwa ushirikiano na FIFA.

Mojawapo ya malengo makuu ya Ligi ya Soka ya Afrika (“AFL”) ni kuhakikisha kwamba ubora wa soka la Vilabu vya Afrika unakuwa na ushindani wa kimataifa na unaoweza kibiashara.

Mshindi wa Uzinduzi wa Ligi ya Soka ya Afrika (“AFL”) atapata Tuzo ya Pesa ya dola za Kimarekani milioni 4, sawa na pesa za Kenya shilingi milioni 595.

Pesa zingine za tuzo ni:

Mshindi wa pili: Dola milioni 3

Waliofuzu nusu fainali: dola milioni 1.7 kila mmoja

Waliofuzu robo fainali: dola milioni 1 kila mmoja