Kwa kuangalia umri wangu, kucheza World Cup 2026 itakuwa ngumu sana - Lionel Messi

Messi pia alikariri maneno kama yale ya Ronaldo akisema matumaini ya kurejea kwake barani Ulaya hayana nafasi hata kidogo kwani alishafunga lango la kurejea katika bara hilo.

Muhtasari

•“Sura yangu ya Ulaya imefungwa? Ndiyo. Shukrani kwa Mungu, nilikuwa na kazi isiyo ya kawaida huko Uropa na nikashinda kila kitu ambacho nimekuwa nikitamani." Messi alisema.

Image: INSTAGRAM// LIONEL MESSI

Mshindi wa taji la kombe la dunia nchini Qatar mwaka 2022, Lionel Messi ameweka matumaini yake ya kushiriki katika mashindano hayo ya 2026 nchini Marekani, Canada na Mexico katika hali ya sintofahamu baada ya kuonekana kudokeza kwamba itakuwa ngumu.

Messi alikuwa anafanya mahojiano na jarida la spoti la L’Equipe kuhusu mustakabali wake kisoka haswa baada ya kuweka rekodi ya kushinda taji la kibinafsi la Ballon d’Or kwa mara 8.

Akiulizwa kuhusu mipango yake ya kuiongoza Argentina kwa mara nyingine katika mashindano ya 2026 kombe la dunia, Messi alisema kwamba itakuwa ngumu sana ikizingatiwa kwamba umri wake kipindi hicho utakuwa umeenda sana lakini pia akasema kwamba atasubiri kuona iwapo atakuwa katika fomu nzuri kushiriki.

"Kombe la Dunia 2026? Kwa kuzingatia umri nitakaokuwa wakati huo, inaonekana kuwa ngumu - lakini tutaona…”.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 36 atakuwa na miaka 39 ifikapo 2026.

Kuhusu uwezekano wake kurejea timu yake ya ujanani, Barcelona, Messi aliweka wasi kwa kunukuu maneno kama yale ya Ronaldo kwamba anahisi kabisa soka lake barani Ulaya limekwisha na wala hakuna mipango yoyote ya kurejea katka timu yoyote achilia mbali Barca.

“Sura yangu ya Ulaya imefungwa? Ndiyo. Shukrani kwa Mungu, nilikuwa na kazi isiyo ya kawaida huko Uropa na nikashinda kila kitu ambacho nimekuwa nikitamani. Sasa kwa kuwa nimeamua kuja Marekani, sidhani kama nitarejea kucheza Ulaya. Nilitaka kurudi Barca, lilikuwa wazo zuri kuwa huko, familia, kustaafu kwangu huko kama nilivyotaka siku zote… lakini haikuwezekana".