Arteta matatani huku akishtakiwa kwa maneno aliyofoka baada ya Arsenal kupigwa na Newcastle

Kocha huyo amepewa hadi Jumanne, Novemba 21 kujibu shtaka dhidi yake kabla ya hatua zaidi kuchukuliwa.

Muhtasari

•Kocha huyo Mhispania huyo alisema kuwa ilikuwa jambo la “kufedheha kabisa" kwamba VAR haikukataza bao la Anthony Gordon.

•Shirikisho la soka la Uingereza limesema kuwa maneno ya Mikel Arteta yalikuwa ya matusi kwa waamuzi na yanadhuru mchezo.

Mikel Arteta
Mikel Arteta
Image: X

Kocha wa Arsenal Mikel Arteta anaweza kuingia matatani baada ya Shirikisho la Soka la Uingereza (FA) kuamua kumshtaki kuhusu maoni yake ‘hasi’ mapema mwezi huu kufuatia kipigo cha 1-0 kutoka kwa Newcastle.

Baada ya mchuano uliochezwa katika uwanja wa St James Park mnamo Novemba 4, Mhispania huyo alisema kuwa ilikuwa jambo la “kufedheha kabisa" kwamba VAR haikukataza bao la Anthony Gordon.

Katika taarifa yake siku ya Alhamisi, FA ilisema kwamba kocha huyo wa Arsenal ameshtakiwa kwa ukiukaji wa Kanuni ya FA E3.1 kutokana na maoni aliyotoa kwenye mahojiano na vyombo vya habari.

"Mikel Arteta ameshtakiwa kwa ukiukaji wa Sheria ya FA E3.1 kufuatia maoni ambayo aliyatoa kwenye mahojiano na vyombo vya habari baada ya mchezo wa Ligi Kuu wa Arsenal dhidi ya Newcastle United mnamo  Jumamosi, Novemba 4," taarifa ya FA ilisoma.

Zaidi ya hayo, shirikisho hilo la soka lilisema kuwa maneno ya Mikel Arteta yalikuwa ya matusi kwa waamuzi na yanadhuru mchezo.

"Inadaiwa kuwa maoni yake ni utovu wa nidhamu kwani ni matusi kwa wasimamizi wa mechi na/au yanaharibu mchezo na/au yanaleta mchezo katika sifa mbaya," FA ilisema.

Kocha huyo mwenye umri wa miaka 41 sasa amepewa hadi Jumanne, Novemba 21 kujibu shtaka dhidi yake kabla ya hatua zaidi kuchukuliwa.

Wakati wa mchuano uliochezwa mapema mwezi huu, VAR ilifanya ukaguzi mara tatu ili kuona kama mpira ulikuwa haujatoka nje kabla ya krosi ya Joe Willock, ikiwa Joelinton alimfanyia madhambi beki wa Arsenal Gabriel, na kama Anthony Gordon alikuwa ameotea.

Hata hivyo, bao hilo lililofungwa dakika ya 64 bado liliruhusiwa kwani VAR haikuweza kupata sababu yoyote ya kulikataa.

Baada ya mechi, Arteta hakuweza kuficha hasira yake, akisema: "Lazima tuzungumze kuhusu jinsi bao hili lilisimama? Ajabu. Naona aibu. Inabidi sasa niingie hapa na kujaribu kuitetea klabu na tafadhali naomba usaidizi, kwa sababu ni aibu kabisa kwamba lengo hili linaruhusiwa. Ni fedheha kabisa.”

Baadaye, klabu ya Arsenal FC ilitoa taarifa ikisema klabu hiyo iliunga mkono kabisa maoni ya Arteta.

 “Ligi Kuu ni ligi bora zaidi duniani yenye wachezaji bora, makocha na mashabiki ambao wote wanastahili zaidi, yote kutoka kwa uchanganuzi wa nyuma, maelezo yaliyojaribiwa na kuomba msamaha,” ilisoma taarifa hiyo.