Man United mbioni kumfuta kazi meneja Erik ten Haag

Meneja huyo amepoteza uungwaji mkono wa takriban 50% ya wachezaji wa Man United.

Muhtasari

•Baadhi yawachezaji wameanza kutilia shaka mtindo wa uchezaji wa meneja huyo na jinsi winga Mwingereza, Jadon Sancho alivyotendewa.

•Ten Haag amedaiwa kuyazibia masikio mashauri yote na ameendelea kufanya mambo kwa njia yake kama dikteta.

Erik ten Hag
Erik ten Hag
Image: EURO SPORT

Mambo yanaripotiwa kutokuwa mazuri katika klabu ya Manchester United huku meneja Erik ten Haag akidaiwa kujipata katika matatizo na baadhi ya wachezaji muhimu.

Kwa mujibu wa Chombo cha Habari za Michezo cha Uingereza, Sky Sports, meneja huyo kutoka Uholanzi  mwenye umri wa miaka 53 amepoteza uungwaji mkono wa takriban 50% ya wachezaji wa Man United.

Mwanahabari mkuu wa Sky Sports News, Kaveh Solhekol, mnamo siku ya Jumatatu aliripoti kwamba baadhi yawachezaji wameanza kutilia shaka mtindo wa uchezaji wa meneja huyo wa zamani wa Ajax na jinsi winga Mwingereza, Jadon Sancho alivyotendewa.

"Wachezaji wamechanganyikiwa kuhusu kinachoendelea na (ten Haag) amepoteza viungo muhimu katika klabu. Chanzo kimoja kinaniambia kuwa amepoteza takriban 50% ya wachezaji. Wachezaji wachache kabisa hawafurahishwi na mtindo wake wa uchezaji na pia wanahisi kwamba wanafanya mazoezi kwa bidii sana na wanakimbia sana wakati wa mazoezi. Nimeambiwa wachezaji hawajui wanakimbilia nini," Kaveh Solhekol alisema.

Aliongeza, “Pia baadhi ya wachezaji wenye uzoefu wamezungumza na Erik ten Haag ambapo wanahisi kuwa klabu inaenda vibaya. Wamezungumza naye kuhusu uzoefu wao katika klabu zingine kubwa. Wanahisi kwamba anapaswa kuwa wazi kidogo, piausimamizi wake wa mtu unaweza kuwa bora zaidi."

Mwanahabari huyo alidai kuwa meneja huyo hata hivyo ameyazibia masikio mashauri yote na ameendelea kufanya mambo kwa njia yake kama dikteta.

"Pia nimeambiwa kwamba wachezaji wachache wanaamini kwamba yeye ni roboti sana na pia wachezaji wachache hawajafurahishwa na jinsi Jadon Sancho alivyotendewa," alisema.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya klabu ya Manchester United kupoteza mechi yao ya nne katika msimu huu na kushuka tena hadi nambari saba jedwali la kwenye ligi kuu wakiwa na pointi 24 pekee katika michuano 14 ya kwanza ya EPL msimu wa 2023/24.

Siku ya Jumamosi, mashetani wekundu walipoteza 1-0 dhidi ya Newcastle United kwenye Uwanja wa St. James Park kufuatia bao la kuvutia la Antony Gordon.