Al Duhail yavunja kimya kuhusu jeraha la Michael Olunga

Olunga alipata jeraha la misuli ya paja wakati wa mechi ya Ligi ya Mabingwa wa Asia dhidi ya Persepolis Jumanne jioni.

Muhtasari

•Kufuatia hilo, klabu hiyo pia ilithibitisha kuwa Olunga atapumzika kidogo kabla ya kuanza mpango wake wa kurejea mazoezini.

alipata jeraha wakati wa mechi ya Jumanne jioni.
Michael Olunga alipata jeraha wakati wa mechi ya Jumanne jioni.
Image: HISANI

Klabu ya soka ya Qatar Al Duhail imezungumza zaidi kuhusu jeraha la nahodha wa Harambee Stars Michael Olunga Ogada.

Katika taarifa, klabu hiyo ilithibitisha kwamba mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 30 ambaye pia ni mfungaji bora wao alipata jeraha la misuli ya paja wakati wa mechi ya Ligi ya Mabingwa wa Asia dhidi ya Persepolis siku ya Jumanne jioni.

Kufuatia hilo, klabu hiyo pia ilithibitisha kuwa Olunga atapumzika kidogo kabla ya kuanza mpango wake wa kurejea mazoezini.

"Uchunguzi wa kimatibabu ulithibitisha kwamba mshambuliaji wa timu, Michael Olunga, alipata jeraha la msuli wa paja katika mguu wake wa kulia, na kusababisha kukosekana kwake hivi majuzi. Atapumzika kabla ya kuanza mpango wa kurekebisha misuli ili ajiunge tena na vipindi vya mazoezi," taarifa ya Al Duhail ilisema.

Michael Olunga alipata jeraha kwenye mguu wake wa kulia wakati wa kipindi cha pili cha mechi ya Al Duhail dhidi ya Persepolis ya Iran Jumanne jioni.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 30 hakuweza kukamilisha mechi hiyo kwani alilala chini kwa maumivu dakika chache tu baada ya kuifungia klabu yake bao la ushindi.

Kwa upande mwingine, Ilikuwa ni kipindi cha kujivunia kwa nahodha huyo wa timu ya taifa ya Harambee Stars, wakati alipotumia ujuzi wake mdogo wa lugha ya Kijapani kuwasaidia wenzake wa Al Duhail kuwasiliana na refa Mjapani ambaye alikuwa akielekeza mechi yao ya Ligi ya Mabingwa wa Asia dhidi ya Persepolis.

Mwamuzi Jumpei Lida ambaye ana asili ya Japan alikuwa amechaguliwa kuchezesha mchezo huo wa hatua ya 6 bora wa ACL uliochezwa kwenye Uwanja wa Azazi mjini Tehran, Iran.

Wakati mechi hiyo ikiendelea, wachezaji wa Al Duhail ambao wengi wao ni Waarabu walihitaji mwamuzi huyo kueleza uamuzi uliotolewa uwanjani lakini kwa bahati mbaya hawakuweza kuelewana vizuri kutokana na tofauti ya lugha, ndipo mwanasoka huyo wa kimataifa wa Kenya alipoingilia kati na kusaidia katika kutatua tatizo hilo.

"Katika mechi ya jana ya ACL, mwamuzi alikuwa Mjapani, lakini kutokana na Kijapani nilichosoma kidogo, niliweza kuwasiliana kwa niaba ya wachezaji wenzangu," Michael Olunga alisema kwa fahari kwenye akaunti yake ya Twitter Jumatano asubuhi.

Aliambatanisha maelezo yake na picha yake akionekana kufanya mazungumzo na mwamuzi wa Japan huku wachezaji wenzake wakitazama na kusikiliza kwa kuchanganyikiwa.