Reece James afanyiwa upasuaji kufuatia jeraha, alalamikia chuki aliyopokea baada ya kujeruhiwa

Msimu wa EPL 2023/24 umekuwa mgumu sana kwa James ambaye amecheza mechi 8 pekee kati ya 17 zilizochezwa.

Muhtasari

•James alifichua alifanyiwa upasuaji ili kurekebisha kabisa tatizo ambalo limekuwa likijirudia katika miezi ya hivi majuzi.

•Alilalamika kuhusu mashambulio na chuki aliyopokea kwenye mitandao ya kijamii baada ya kupata jeraha tena.

Image: INSTAGRAM// REECE JAMES

Nahodha wa klabu ya soka ya Chelsea, Reece James ametoa taarifa kuhusu afya yake takriban wiki mbili baada ya kutolewa uwanjani kutokana na jeraha.

James alikuwa amecheza kwa dakika 27 pekee wakati wa mechi ya Chelsea dhidi ya Everton mnamo Desemba 12 kabla ya kutolewa nje baada ya jeraha la mguu alilopata kumfanya ashindwe kuendelea kucheza.

Katika taarifa yake ya Alhamisi jioni, beki huyo mwenye umri wa miaka 24 alifichua kwamba alifanyiwa upasuaji ili kurekebisha kabisa tatizo ambalo limekuwa likijirudia katika miezi ya hivi karibuni na kumfanya ashindwe kucheza.

"Ulimwengu wa kandanda ulijua nilijeruhiwa lakini utaratibu ambao ningefanya wakati huu ulichukua muda mrefu zaidi kupata suluhisho bora," Reece James alisema kupitia ukurasa wake wa Instagram Alhamisi jioni.

Aliambatanisha taarifa yake na picha yake akiwa amelazwa kwenye kitanda cha hospitali huku akiinua kidole gumba chake cha kushoto kuashiria anaendelea vizuri.

"Nilifanyiwa upasuaji leo (Alhamisi)  ili kujaribu kurekebisha tatizo langu la misuli ya paja lililokuwa linajirudia, afueni imeanza, kimwili na kiakili," aliongeza.

Mwanasoka huyo wa Kimataifa wa Uingereza aliendelea kulalamika kuhusu mashambulio na chuki aliyopokea kwenye mitandao ya kijamii baada ya kupata jeraha tena mapema mwezi huu.

"Tangu jeraha hili nimekuwa na usaidizi mzuri lakini kikubwa zaidi ni chuki na mashambulio. Niamini, sitaki kujeruhiwa. Nina furaha zaidi ninapocheza soka," alisema.

Aliongeza, "Shukrani kwa watu wanaoelewa ambao wananiunga mkono licha ya hali ya juu au ya chini, inaenda mbali".

Msimu wa EPL 2023/24 umekuwa mgumu sana kwa nahodha huyo wa Chelsea ambaye amecheza mechi nane pekee kati ya kumi na saba ambazo klabu hiyo imecheza.

Beki huyo mwenye umri wa miaka 24 ametumia muda mwingi wa msimu akipambana na jeraha na akiwa amehudumia marufuku ya kadi nyekundu, na hivyo kufanya iwe vigumu kwake kupata dakika uwanjani.