Beki wa Kenya Eric 'Marcelo' Ouma kulipwa mamilioni baada ya kusainiwa na miamba wa soka wa Poland

Erick amesaini mkataba wa miaka mitatu na mabingwa hao wa ligi ya Poland msimu uliopita.

Muhtasari

•Erick alitambulishwa rasmi kama mchezaji mpya wa Rakow siku ya Alhamisi na akathibitisha kuwa amefurahishwa na hatua hiyo kubwa.

•AIK itapata takriban Ksh150m kutokana na mauzo ya beki huyo wa kushoto huku 30% ikienda kwa klabu yake ya zamani, Vasalunds IF.

amejiunga na Rakow
Eric Ouma amejiunga na Rakow
Image: HISANI// RAKOW

Beki mahiri wa Harambee Stars, Eric ‘Marcelo’ Ouma amejiunga na miamba ya soka ya Poland Rakow Czestochowa kutoka klabu ya AIK Fotbol ya Uswidi.

Erick alitambulishwa rasmi kama mchezaji mpya wa klabu hiyo iliyoshiriki katika Europa League 2023/24 siku ya Alhamisi na akathibitisha kuwa amefurahishwa na hatua hiyo kubwa.

"Poland ni ligi nzuri kwa kweli. Ninajivunia kuwa hapa, kuwa katika timu hii kubwa ambayo kwa kweli inafanya vizuri na inacheza soka nzuri,” Erick alisema kwenye mahojiano baada ya kusaini mkataba wake mpya.

Aliongeza, "Nadhani Poland na Uswidi ni sawa. Aina ya hali ya hewa na kila kitu, nadhani zinafanana kwa hivyo kwangu, nina furaha."

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Kenya mwenye umri wa miaka 27 alimsifu kocha wa Rakow, Szwarga D. na kusema anatazamia kucheza chini yake.

Erick ambaye amekuwa akicheza nchini Uswidi tangu 2020 ametia saini mkataba wa miaka mitatu na mabingwa hao wa ligi ya Poland mwaka jana ambao utaisha 2026. Mkataba wake pia unajumuisha chaguo la kuongeza miaka miwili.

Inaripotiwa kuwa AIK itapata takriban Ksh150m kutokana na mauzo ya beki huyo wa kushoto mwenye umri wa miaka 27 huku 30% yake ikienda kwa klabu yake ya zamani, Vasalunds IF.

Kulingana na vyombo vya habari vya Poland, mchezaji wa Harambee Stars atakuwa akipokea pauni 7300 kwa wiki (takriban Ksh1.5milioni) ambayo ina maana atakuwa akienda nyumbani na takriban Ksh6milioni kwa mwezi.

Sote tunamtakia Eric mafanikio mema anapoanza safari yake mpya nchini Uswidi.