"Huru!" Mshambuliaji Ivan Toney asherehekea baada ya marufuku ya miezi 8 kuisha

Toney alipigwa marufuku mnamo Mei 17, 2023 baada ya kukubali mashtaka ya kuvunja sheria za kamari za Shirikisho la Soka.

Muhtasari

•Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 27 alishiriki video aina ya gif ya mwanamume akionekana kusherehekea uhuru wake.

•Toney pia alikuwa ametozwa £50,000 na kuonywa kuhusu mwenendo wake wa baadaye kwa ukiukaji 232 wa sheria za kamari za FA.

Image: INSTAGRAM// IVAN TONEY

Mshambulizi wa Brentford na Uingereza, Ivan Toney, hakuweza kuficha furaha yake baada ya marufuku yake ya kutojihusisha na soka kwa miezi minane kuisha siku ya Jumatano.

Toney alipigwa marufuku kutoka kwa shughuli zote za kandanda kwa miezi minane mnamo Mei 17, 2023 baada ya kukubali mashtaka ya kuvunja sheria za kamari za Shirikisho la Soka. Marufuku hiyo ilitakiwa kuisha Januari 17, 2024 na baada ya hapo angeruhusiwa kurejea uwanjani.

Wakati akisherehekea mwisho wa marufuku yake siku ya Jumatano, mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 27 alishiriki video aina ya gif ya mwanamume akionekana kusherehekea uhuru wake.

“Huru!” gif ilisoma.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Uingereza sasa yuko huru kuichezea klabu yake ya Brentford katika mechi inayofuata huku mustakabali wake ukiendelea kujadiliwa. Amekuwa akihusishwa sana na uhamisho kwenda Arsenal au Chelsea huku klabu hizo mbili za London zikiripotiwa kumtaka

Zaidi ya kupigwa marufuku kwa miezi minane, Toney pia alikuwa ametozwa £50,000 na kuonywa kuhusu mwenendo wake wa baadaye kwa ukiukaji 232 wa sheria za kamari za FA.

Marufuku yake ilianza Mei 17 mwaka jana, lakini mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27 aliruhusiwa kurejea mazoezini na Brentford miezi minne kabla ya mwisho wa marufuku, ambayo ilikuwa ni Septemba 18.

Wakati akizungumza kwenye ukurasa wake wa Instagram baada ya uamuzi huo kutolewa mwaka jana, Toney alisema "amesikitishwa kiasili" na uamuzi huo, na hangetoa maoni zaidi hadi Tume huru ya Udhibiti itakapochapisha sababu zake zilizoandikwa.

"Sitoi maoni zaidi kwa wakati huu zaidi ya kuwashukuru familia yangu na marafiki, Brentford FC na mashabiki wetu kwa kuendelea kutuunga mkono, katika kipindi kigumu sana.

"Sasa nazingatia kurejea kucheza mchezo ninaoupenda msimu ujao."

Katika taarifa, FA ilisema: "Marufuku yake[Toney] iliwekwa na Tume huru ya Udhibiti baada ya kusikilizwa kwa kesi. Sababu za maandishi za Tume huru ya Udhibiti za marufuku haya zitachapishwa kwa wakati ufaao, na FA itasubiri kuzipitia kabla ya kutoa maoni zaidi."

Ukiuakaji ulioripotiwa wa Toney ulifanyika kati ya 25 Februari 2017 na 23 Januari 2021, wakati ambapo Toney aliwakilisha Scunthorpe United, Wigan Athletic, Peterborough United na Brentford.