Afcon 2023: Taifa stars ya Tanzania yacharazwa mabao 3 bila jibu na Morocco

Tanzania ilipata pigo kubwa baada ya mchezaji wake Novatus Miroshi kupigwa kadi nyekundu kunako dakika ya 72.

Muhtasari

• Wachezaji wa Morocco , Hakim Ziyech, Ounahi na Youssef el Nasri walikuwa moto wa kuotea mbali kwa timu ya Tanzania .

Wachezaji wa Morocco wakisherehekea ushindi wao dhidi ya Tanzania
Wachezaji wa Morocco wakisherehekea ushindi wao dhidi ya Tanzania
Image: BBC

Timu ya Tanzania Taifa Stars imecharazwa magoli matatu kwa bila katika mechi iliokamilika huku Tanzania ikisalia na wachezahi 10 uwanjani.

Morocco ambao waliwakilisha bara la Afrika katika kombe la Dunia la 2022, ilitawala mchezo huo kuanzia dakika ya kwanza hadi ya mwisho.

Kufikia mwisho wa kipindi cha kwanza, Morocco ambayo ilikuwa inaongoza kwa goli lililofungwa na nahodha Romain Saiss , walikuwa wameshambulia mara 8 huku wapinzani wao wakishindwa kushambulia hata mara moja.

Na katika kipindi cha pili Tanzania ilipata pigo kubwa baada ya mchezaji wake Novatus Miroshi kupigwa kadi nyekundu kunako dakika ya 72.

Tanzania hata hivyo ilijitahidi na kujaribu kushmbulia kutoka mbali baada ya kushindwa kupenya katika safu ya ulinzi ya Morocco.

Jitihada za mshambuliaji nyota wa Tanzania Mbwana Samatta na mwenzake Msuva kujaribu kuchukua mpira kutoka katikati ya uwanja na kusonga nao mbele ziliambulia patupu huku kiungo wa kati wa Morocco Amrabat akitawala safu ya kati.

Wachezaji wa Morocco , Hakim Ziyech, Ounahi na Youssef el Nasri walikuwa moto wa kuotea mbali kwa timu ya Tanzania .

Na haikuchukua muda mrefu kabla ya mchezaji Ounahi kuipatia bao la pili Morocco.

Na baadaye Youssef En-Nesyri alifunga krosi iliopigwa na Achraf Hakimi ili kujipatia ushindi huo wa mabao matatu kwa bila baada ya bao hilo kuchunguzwa na VAR na kuthibitishwa.