Ghana yamfuta kocha kufuatia matokeo duni kwenye AFCON 2023

Houghton alitimuliwa siku moja tu baada ya The Black Stars kutoka sare ya kushangaza dhidi ya Msumbiji

Muhtasari

•Shirikisho la Soka la Ghana pia lilivunja timu nzima ya ufundi katika harakati za kurekebisha usimamizi wa timu ya taifa.

•Ghana ilimaliza ya tatu katika Kundi B la AFCON 2023 baada ya kufanikiwa kupata pointi mbili pekee kutokana na mechi zilizochezwa.

amefutwa kazi
Kocha Chris Houghton amefutwa kazi
Image: GFA

Shirikisho la Soka la Ghana (GFA) limemfuta kazi kocha mkuu wa Black Stars, Chris Houghton.

Shirikisho hilo lilitangaza kuhusu kutimuliwa kwa Houghton mnamo usiku wa kuamkia Jumatano, siku moja tu baada ya The Black Stars kutoka sare ya kushangaza dhidi ya Msumbiji.

Pamoja na kumfukuza kazi meneja huyo wa soka kutoka Ireland, Ghana pia ilivunja timu nzima ya ufundi katika harakati za kurekebisha usimamizi wa timu ya taifa.

"Shirikisho la Soka la Ghana linapenda kutangaza kwamba Chris Hughton ameondolewa majukumu yake kama kocha mkuu wa timu ya Taifa ya wakubwa mara moja," GFA ilisema katika taarifa Jumanne usiku.

"Baraza la Utendaji pia limechukua uamuzi wa kuvunja timu ya ufundi ya Black Stars. Chama cha Soka cha Ghana katika siku zijazo kitatoa ramani ya mwelekeo wa siku zijazo wa Black Stars," taarifa hiyo ilisema zaidi.

Hatua hii imekuja siku moja tu baada ya The Black Stars kushindwa kushinda mechi yao ya tatu katika hatua ya makundi ya AFCON 2023, na hivyo kupunguza nafasi zao za kufuzu hadi raundi inayofuata. Sare ya 2-2 dhidi ya Msumbiji mnamo Jumatatu usiku ilikuwa mechi yao ya tano mfululizo bila ushindi.

Ghana ilimaliza ya tatu katika Kundi B la AFCON 2023 baada ya kufanikiwa kupata pointi mbili pekee kutokana na mechi zilizochezwa.

Katika mchuano wa kwanza, walipoteza 1-2 na Cape Verde mnamo Januari 14, wakatoka sare ya 2-2 dhidi ya Misri Januari 18 kabla ya kutoka sare ya 2-2 tena dhidi ya Msumbiji.

Kulikuwa na matarajio makubwa sana kutoka kwa timu ya Ghana yenye uzoefu lakini kuna uwezekano mkubwa kwamba hawatafuzu kwa awamu inayofuata ya Afcon.