Kocha ​​Xavi atangaza mipango ya kuondoka Barcelona kufuatia kichapo cha 3-5 na Villareal

Xavi alisema hataendelea kuisimamia klabu hiyo zaidi ya Juni 30 mwaka huu.

Muhtasari

•Meneja huyo mwenye umri wa miaka 44 alitoa tangazo hilo siku ya Jumamosi jioni kufuatia kichapo cha aibu cha Barcelona cha 3-5 dhidi ya Villareal.

•Alisema kuondoka ni uamuzi bora kwani miamba hao wa Uhispania wanaonekana kutokuwa kwenye njia sahihi kwa sasa.

Xavi Hernandez
Image: BBC

Kiungo wa zamani wa Barcelona ambaye ni meneja wa sasa wa wababe hao wa Uhispania, Xavi Hernandez ametangaza kuwa ataondoka katika klabu hiyo mwishoni mwa msimu wa 2023/24.

Meneja huyo mwenye umri wa miaka 44 alitoa tangazo hilo siku ya Jumamosi jioni kufuatia kichapo cha aibu cha Barcelona cha 3-5 dhidi ya Villareal.

Xavi alisema hataendelea kuisimamia klabu hiyo zaidi ya Juni 30 mwaka huu, ingawa mkataba wake utaendelea hadi majira ya joto yanayofuata.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari baada ya mechi, bosi huyo wa Barcelona alisema, "Nitaondoka Barcelona mwezi Juni. Tumefikia hatua ya kutorudi nyuma. Ni wakati wa mabadiliko. Kama kocha, nadhani ni wakati wa kuondoka. Nilizungumza. na bodi na klabu leo (Jumamosi). Nitaondoka tarehe 30 Juni."

Alisema kuondoka katika klabu hiyo ambayo ameiongoza tangu Novemba 2021 ni uamuzi bora kwani miamba hao wa Uhispania wanaonekana kutokuwa kwenye njia sahihi kwa sasa.

"Nilichukua uamuzi huu siku zilizopita. Tayari nilijua. Lakini ni wakati wa kuiweka hadharani. Nadhani wachezaji hawakuweza kujiweka huru. Sitaki kuwa tatizo kwa klabu, lakini kinyume chake. Hivi sasa, nikifikiria kwa kichwa na kufikiria kuhusu klabu, suluhu na jambo bora ni kuondoka Juni, ndivyo ninavyojisikia,” alisema.

Aliongeza, “Tumekubaliana hilo na rais (Joan Laporta). Tuna rais mwenye kipaji. Yeye, Rafa Yuste, (mkurugenzi wa michezo), Deco…kila mtu ana uwezo. Nadhani uamuzi huu utasaidia kufungua timu na hali hapa. Nilimwambia rais Laporta sasa tayari.. Tumekuwa na mkutano, yalikuwa mazungumzo ya kibinadamu sana, kwa akili ya kawaida tu. Imani kutoka kwao bado ni nzuri.”

Kiungo huyo wa zamani wa Barcelona na Uhispania alianza kuisimamia klabu hiyo Novemba 2021 baada ya kuondoka katika klabu ya Al Sadd ya Qatar.

Aliiongoza Barca kutwaa ubingwa wa Laliga katika msimu wake wa kwanza kamili msimu wa 2022-23, lakini kichapo cha Jumamosi 5-3 nyumbani kutoka kwa Villarreal kinawaacha pointi 10 nyuma ya vinara wa La Liga Real Madrid.