Afcon 2023: Miamba waanguka huku kombe likiingia robo fainali, fahamu nani walifuzu

Afrika Kusini na Mali zinaungana na Nigeria, Angola, D.R Congo, Guinea, Ivory Coast na Cape Verde katika robo fainali.

Muhtasari

•Afcon 2023 imeingia hatua ya robo fainali baada ya mechi mbili za mwisho za hatua ya 16 bora kuchezwa Jumanne jioni.

• Afrika Kusini wakiwacharaza washindi wa AFCON 2019, Morocco mabao 2-0 na kuwatoa nje ya kombe hilo la kifahari la Afrika.

usiku wa Jumanne.
Morocco walibanduliwa nje ya kombe usiku wa Jumanne.
Image: AFCON 2023

Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika 2023 (AFCON) inayoendelea nchini Ivory Coast imeingia hatua ya robo fainali baada ya mechi mbili za mwisho za hatua ya 16 bora kuchezwa Jumanne jioni.

Siku ya mwisho ya hatua ya 16 bora ilishuhudia timu ya Bafana Bafana ya Afrika Kusini wakiwacharaza washindi wa AFCON 2019, Atlas Lions wa Morocco mabao 2-0 na kuwatoa nje ya kombe hilo la kifahari la Afrika. Mshambulizi Evidence Makgopa na kiungo Teboho Mokoena walifunga katika kipindi cha pili cha mechi hiyo na kuipa Bafana Bafana ushindi huo wa kushtukiza.

Morocco ilikuwa imefunga bao kupitia Abde Ezzalzouli katika kipindi cha kwanza lakini likakataliwa baada ya mshambuliaji huyo kuamuliwa kuwa ameotea. Staa wa PSG Achraf Hakimi pia alikosa penalti katika kipindi cha pili huku Sofyan Amrabat wa Manchester United akipewa kadi nyekundu kuelekea mwisho wa mechi baada ya kucheza vibaya.  

Mapema Jumanne usiku, Mali ilimenyana na Burkina Faso na kuwafunga 2-1 na kuwafanya kuwa timu ya saba kufuzu kwa robo fainali ya AFCON 2023. Bao la kujifunga kutoka kwa beki Edmond Tapsoba na fowadi Lassine Sinayoko liliipa Mali ushindi huku nahodha Bertrand Traore akifunga bao pekee la Burkina Faso.

Afrika Kusini na Mali sasa zinaungana na Nigeria, Angola, D.R Congo, Guinea, Ivory Coast na Cape Verde katika robo fainali itakayochezwa Ijumaa na Jumamosi.

Tazama ratiba ya mechi za robo fainali Afcon 2023:

Nigeria vs Angola  (Ijumaa, Saa mbili usiku masaa ya Afrika Mashariki kwenye uwanja wa Stade Felix Houphouet-Boigny)

D.R Congo vs Guinea (Ijumaa, Saa tano usiku masaa ya Afrika Mashariki kwenye uwanja wa Stade Olympique Alassane Quattara.

Mali vs Ivory Coast (Jumamosi, Saa mbili usiku masaa ya Afrika Mashariki kwenye uwanja wa Stade de la Paix (Bouake)

Cape Verde vs South Africa (Jumamosi, Saa tano usiku masaa ya Afrika Mashariki kwenye uwanja wa Charles Konan Banny, Yamoussoukro)