"Mmetuua!” Winga wa Senegal akasirika, alia ufisadi baada ya kuchapwa na Ivory Coast

“Mmetuua, mafisadi! Wekeni Kombe lenu la Afrika,” Diatta alisema.

Muhtasari

•Krepin Diatta hakuchukulia mambo kirahisi sana baada ya Lions of Teranga kuondolewa kwenye (AFCON siku ya Jumatatu usiku.

•Mshambulizi huyo alienda akikashifu Shirikisho la Soka Afrika, akiwashutumu maafisa wake kwa ufisadi.

Mshambulizi Krepin Diatta
Image: HISANI

MSHAMBULIAJI wa Senegal, Krepin Diatta hakuchukulia mambo kirahisi sana baada ya Lions of Teranga kuondolewa kwenye Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) siku ya Jumatatu usiku.

Mabingwa hao watetezi walilazimika kuondoka katika michuano hiyo katika hatua ya 16 bora baada ya wenyeji Ivory Coast kutoka nyuma na kusababisha sare, kabla ya baadaye kuwafunga kwa mikwaju ya penalti katika mechi hiyo kali na ya kihisia iliyochezwa kwenye Uwanja wa Charles Konan Banny.

Kufuatia kipigo hicho cha aibu, Diatta ambaye pia anachezea klabu ya Monaco ya Ufaransa hakuonekana kuwa na furaha hata kidogo alipokuwa akitoka nje ya uwanja kwani alienda akikashifu Shirikisho la Soka Afrika, akiwashutumu maafisa wake kwa ufisadi.

“Mmetuua, mafisadi! Wekeni Kombe lenu la Afrika,” Diatta alisema.

Aliongeza, "Samahani, lakini ni ujinga. Samahani sana, lakini wameua mashindano yetu hapo."

Senegal walikuwa wametangulia kufunga kupitia mshambulizi Habib Diallo katika mechi iliyochezwa Jumanne usiku. Mechi hiyo nusura ionekane kumalizikia kwa ushindi wa Lions of Teranga kabla ya kiungo wa Al Ahli SC, Franck Kessie kufunga bao kwa wenyeji na kufanya mchezo huo kuwa sare ya 1-1.

Mechi hiyo ilienda bila bao katika muda wa ziada na mshindi alilazimika kuamuliwa kupitia mikwaju ya penalti ambapo Ivory Coast walifunga nafasi zote lakini mlinzi wa Senegal Moussa Niakhate alipoteza nafasi yake ya kumaliza mechi kwa 5-4 kwa penalti.