Beki Dani Alves afungwa jela miaka 4 na nusu baada ya kupatikana na hatia ya ubakaji

Pia amehukumiwa miaka mitano zaidi ya uhuru wa ‘kusimamiwa’ baada ya kuachiliwa kutoka gerezani.

Muhtasari

•Mahakama ilimpata beki huyo na hatia ya kumbaka mwanamke katika klabu ya usiku jijini Barcelona mnamo Desemba 31, 2022.

•Dani Alves alikamatwa mnamo Januari 2023 na amekuwa akizuiliwa tangu wakati huo baada ya maombi ya dhamana kukataliwa.

amefungwa jela miaka minne unusu
Beki Dani Alves amefungwa jela miaka minne unusu
Image: HISANI

Mchezaji wa zamani wa Barcelona na timu ya taifa ya Brazil Dani Alves atatumikia kifungo cha miaka minne na nusu jela.

Hii ni baada ya mahakama moja nchini Uhispania kumpata beki huyo mwenye umri wa miaka 40 na hatia ya kumbaka mwanamke katika klabu ya usiku jijini Barcelona mnamo Desemba 31, 2022.

Kando na kifungo hicho, pia ameagizwa kumlipa mwathiriwa pauni 128,500 (Ksh 23.8milioni). Pia amehukumiwa miaka mitano zaidi ya uhuru wa ‘kusimamiwa’ baada ya kuachiliwa kutoka gerezani.

Raia huyo wa Brazil pia haruhusiwi kwenda umbali wa kilomita moja karibu na mwathiriwa wake na hawezi kuwasiliana na mwanamke huyo kwa miaka tisa.

Dani Alves alikamatwa mnamo Januari 2023 na amekuwa akizuiliwa tangu wakati huo baada ya maombi ya dhamana kukataliwa.

Waendesha mashtaka walikuwa wakitaka kifungo cha miaka tisa jela kwa mwanasoka huyo wa zamani.

Waendesha mashtaka walisema Alves na rafiki yake walinunua shampeni kwa wasichana watatu kabla ya kumvuta mmoja wao hadi kwenye eneo la VIP la klabu hiyo ya usiku bila idhini yake.

Walisema kuwa ni wakati huu ambapo Alves aligeuka kuwa mkali, na kumlazimisha mwanamke huyo kufanya ngono licha ya maombi yake ya mara kwa mara ya kuondoka.

Alves alikuwa ameshikilia kuwa mwanamke huyo angeweza kuondoka "kama angetaka". Walakini, mahakama iligundua kuwa hakukubali.

Katika taarifa, mahakama ilisema kulikuwa na ushahidi zaidi ya ushuhuda wa mwathiriwa ambao ulithibitisha kuwa alibakwa.

Ilisema Alves "alimshika mlalamishi ghafla" na kumtupa chini. Kisha alimbaka huku akimzuia kusonga kwani "mlalamishi alisema hapana na alitaka kuondoka", iliongeza.

Mwanamke huyo alisema ubakaji huo ulimsababishia "uchungu na woga", na mmoja wa marafiki zake ambaye alikuwa naye usiku huo alielezea jinsi msichana huyo wa miaka 23 alilia "bila kujizuia" baada ya kutoka bafuni.

Alves amekuwa kizuizini kabla ya kesi yake kusikizwa tangu Januari 2023 na amebadilisha ushuhuda wake mara kadhaa.

Alves aliichezea Barcelona zaidi ya mara 400, akishinda mataji sita ya ligi na Ligi ya Mabingwa mara tatu kwa misimu miwili akiwa na klabu hiyo.

 Pia alikuwa sehemu ya kikosi cha Brazil cha Kombe la Dunia la 2022.