Liverpool vs Man City: Tazama ushindani wa Jurgen Klopp na Pep Guardiola Uingereza

Ushindani wao wa Ligi ya Kuu ya Uingereza unaweza kumaliza kwa mchezo wa siku ya Jumapili.

Muhtasari

•Mameneja hao wamepigana vita vikubwa vya kuwania taji - na ushindani wao wa Ligi ya Kuu ya Uingereza unaweza kumaliza kwa mchezo wa siku ya Jumapili.

Image: BBC

Ushindani wa Jurgen Klopp, Meneja wa Liverpool na mwenzake wa Manchester City, Pep Guardiola umetawala lakini pia umebadilisha soka la Uingereza.

Mameneja hao wamepigana vita vikubwa vya kuwania mataji - na ushindani wao wa Ligi ya Kuu ya Uingereza unaweza kumaliza kwa mchezo wa siku ya Jumapili.

Vinara Liverpool watakapowakaribisha Manchester City, huku mshindi akitarajiwa kuwa kileleni, na sare inaweza kumfungulia milango Arsenal ilio nafasi ya tatu.

Guardiola huenda hana mpango wa kwenda popote hivi karibuni - lakini Klopp aliushangaza ulimwengu wa soka alipotangaza Januari kwamba ataondoka Liverpool mwishoni mwa msimu huu.

Mafanikio Yao

Orodha ya Vikombe
Image: BBC

Liverpool ya Klopp ndiyo timu pekee imesimama katika njia ya City ya kutwaa taji la Ligi Kuu ya Uingereza.

Klopp aliwasili Anfield Oktoba 2015, akichukua nafasi ya Brendan Rodgers aliyetimuliwa, na akatangaza "kama nitakaa hapa baada ya miaka minne, nina imani tutakuwa na taji japo moja."

Ilimchukua miaka minne na nusu - lakini ilimaliza kusubiri kwa miaka 30 kwa Liverpool iliyochukua taji la 2019/20.

Miezi tisa baada ya Klopp kuhamia Uingereza, takribani maili 35 kutoka Anfield, Guardiola alionekana kwenye Uwanja wa Etihad.

City walimaliza wa tatu katika mwaka wa kwanza wa Guardiola lakini wakashinda mataji matano kati ya sita yaliyofuata.

Mabosi wote wawili wameshinda kila kombe - Ligi Kuu, Kombe la FA, Kombe la Carabao, Ngao ya Jamii, Ligi ya Mabingwa, Uefa Super Cup na Kombe la Dunia la Vilabu la Fifa.

Chochote kitakachotokea Jumapili, Klopp ataondoka England akiwa na faida - akiishinda City mara nane kati ya mechi 21, dhidi ya sita za Guardiola.

Ushindani wa Heshima

Image: BBC

Kuna ushindani wa kudumu kama uliokuwepo kati ya Alex Ferguson na Arsene Wenger, au Wenger na Jose Mourinho, au Mourinho na Antonio Conte.

Mechi yao ya mwisho ya ligi ilikuwa sare ya 1-1 huko Etihad mwezi Novemba. Klopp na Guardiola ambao wote wanazungumza Kihispania, mara nyingi husifiana kila mmoja katika mikutano na wanahabari na mahojiano.

Mara nyingi, Klopp humtaja Guardiola kama meneja bora zaidi duniani. "Mimi na Pep sio marafiki wakubwa kwa sababu hatufahamiani lakini ninamheshimu sana na najua anaheshimu tunachofanya pia. Ni ushindani, na hatuhitaji kudharauliana," Mjerumani huyo alisema.

Guardiola, alisema 2021 "timu yake (Pep) imenisaidia mimi kuwa meneja bora. Yaani kuifikiria timu yake, kuishinda na kuwa meneja bora."

"Hiyo ndiyo sababu bado niko katika biashara hii. Baadhi ya mameneja - na Jurgen ni mmoja wao - wanakupa changamoto kupiga hatua mbele."

Guardiola, alipokuwa bosi wa Barcelona, alikuwa akichuana vikali na kocha wa Real Madrid, Mourinho kwa miaka kadhaa.

Lakini alisema: "Jurgen, kama meneja, amekuwa mpinzani mkubwa zaidi niliyewahi kukutana naye katika kazi yangu.

"Sio kumdhihaki Jose. Ni meneja wa kuvutia na nilikuwa mpinzani wake lakini nimecheza mechi nyingi zaidi dhidi ya Liverpool."

Ushindani ulioanzia Ujerumani

Wawili hao pia walikuwa na misimu miwili pamoja Ujerumani - wakifundisha wapinzani wakubwa Bayern Munich na Borussia Dortmund.

Guardiola akiwa bado Barcelona, Klopp aliiongoza Dortmund na kuiongoza kutwaa ubingwa wa Bundesliga msimu wa 2010-11 na 2011-12.

Mchezo wa kwanza wa Guardiola kama mkufunzi wa Bayern Julai 2013 ulikuwa dhidi ya Klopp katika Kombe la Super Cup la Ujerumani, Borussia Dortmund ilishinda 4-2.

Hata hivyo, Bayern walitwaa ubingwa wa Bundesliga na kuwashinda Dortmund katika fainali ya Kombe la Ujerumani. Mwaka mmoja baadaye Klopp alijiuzulu baada ya kumaliza akiwa nafasi ya saba.

Huku timu zote mbili zikiwa bado kwenye Kombe la FA katika hatua ya robo fainali, zinaweza kumenyana tena Wembley.

Manchester City watakuwa wenyeji wa Newcastle na Liverpool wako Manchester United katika hatua ya nane bora.

Klopp tayari amesema hatofundisha England tena - na ana nia ya kuwa na mapumziko ya mwaka mmoja 2024-25. Baadhi wanaamini kazi yake inayofuata itakuwa ni meneja wa Ujerumani.

Guardiola amebakiza msimu mwingine katika mkataba wake wa City mwishoni mwa huu na amedokeza kuwa atasalia hapo.

Kiungo huyo wa zamani wa Uhispania amesema angependa kusimamia timu ya taifa siku moja, huku Brazil na Uingereza zikiwa miongoni mwa mataifa ambayo amekuwa akihusishwa nayo.