Mashabiki wa Shabana FC wakwea vilimani Ngong kuiombea dhidi ya nuksi ya kupigwa

Mpaka sasa, Shabana FC wameshiriki mechi 24 lakini wamepoteza mechi 14, huku wakishinda mara 4 na kutoka sare mara 6, wakiwa katika nafasi ya pili kutoka mkiani na pointi 18 tu.

Muhtasari

• Klabu hiyo inashikilia nafasi ya 17 kwenye jedwali, ikiwa ni nafasi ya pili kutoka mkiani na pointi 18 tu.

• Gor Mahia wanaongoza jedwali kwa alama 50 wakifuatiwa kwa umbali na Tusker FC yenye pointi 43.

 

MASHABIKI WA SHABANA
MASHABIKI WA SHABANA
Image: HISANI

Jumapili, sehemu ya mashabiki wa klabu ya Shabana FC yenye mizizi yake kutoka eneo la Gusii walijukumika katika vilima vya Ngong, kaunti ya Kajiado kuiombea timu hiyo dhidi ya nuksi ya kugaragazwa kama ngoma katika takribani kila mchezo wanaoshiriki.

Katika picha ambazo zimeenezwa mitandaoni, mashabiki hao walikuwa wamevalia jezi za timu hiyo pendwa ya Gusii na walionekana wakifanya ibada huku wamepiga magoti na kuinua mikono juu.

Inaarifiwa kwamba lengo kuu la mkutano huo wa kiimani lilikuwa ni kuiombea timu hiyo ili kupata matokeo mema katika ligi kuu ya FKF katika juhudi za kusalia kwenye ligi msimu ujao.

Mpaka sasa, Shabana FC wameshiriki mechi 24 lakini wamepoteza mechi 14, huku wakishinda mara 4 na kutoka sare mara 6.

Klabu hiyo inashikilia nafasi ya 17 kwenye jedwali, ikiwa ni nafasi ya pili kutoka mkiani na pointi 18 tu.

Gor Mahia wanaongoza jedwali kwa alama 50 wakifuatiwa kwa umbali na Tusker FC yenye pointi 43.

Shabana FC ilipanda daraja kutoka ligi ya NSL mwanzoni mwa msimu huu lakini wameshindwa kuweka matokeo ya kufurahisha kwa maelfu ya mashabiki wao.

Shabana FC inatajwa kuwa timu ya tatu yenye mashabiki wengi nchini baada ya Gor Mahia na AFC Leopards.

Itakumbukwa siku chache zilizopita wakati wa kusherehekea miaka 60 ya klabu ya AFC LLeopards, rais William Ruto alimuagiza waziri wa michezo Ababu Namwamba kuunda jopokazi la kuhakikisha vilabu hivyo vitatu – Gor Mahia, AFC Leopards na Shabana FC wanatengewa ardhi ya kujenga viwanja vyao, kwani wana mashabiki wengi katika soka ya humu nchini.

Je, Shabana FC itabahatika kusalia kwenye ligi ya FKF ama itashuka na kurudi kwenye NSL?