•Nottingham Forest ilipata pigo kubwa Jumatatu jioni baada ya kupokonywa pointi nne kutoka kwa jumla ya pointi zao msimu huu.
•Klabu ilielezea kusikitishwa kwake na mashtaka na ushahidi uliowasilishwa dhidi yao na ligi kuu ikitaja kuwa hayakutarajiwa.
Siku ya Jumatatu jioni, klabu ya soka ya Nottingham Forest ilipata pigo kubwa baada ya kupokonywa pointi nne kutoka kwa jumla ya pointi zao msimu huu.
Klabu hiyo yenye maskani yake Nottinghamshire ilikabiliwa na adhabu hiyo baada ya tume ya Ligi Kuu kuipata na hatia ya kukiuka kanuni za faida na uendelevu.
Katika taarifa iliyotolewa baada ya adhabu hiyo, klabu hiyo ilieleza kusikitishwa kwake na uamuzi huo ulioirudisha hadi nambari 18 kwenye jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza ikiwa na pointi 21 pekee kati ya mechi 29 ilizocheza.
"Nottingham Forest imesikitishwa sana na uamuzi wa Tume ya kuweka adhabu kwa Klabu ya kupokonywa pointi nne, kutumika mara moja," taarifa iliyochapishwa na Nottingham Forest kwenye tovuti yake rasmi ilisomeka.
Ilisomeka zaidi, “Pamoja na kusikitishwa kwetu, tunaishukuru Tume kwa kukubali kushughulikia suala hili kwa haraka. Klabu inaona kuwa ni muhimu kwa uadilifu wa ligi kusuluhisha mashtaka katika msimu ambao yatatolewa."
Klabu hiyo pia ilielezea kusikitishwa kwake na mashtaka na ushahidi uliowasilishwa dhidi yao na ligi kuu ikitaja kuwa hayakutarajiwa.
"Baada ya miezi kadhaa ya mazungumzo na Ligi Kuu, na ushirikiano wa kipekee wakati wote, hii haikutarajiwa na imeharibu imani na imani tuliyokuwa nayo katika Ligi Kuu," ilisema.
Klabu hiyo sasa imedokeza kuhusu kukata rufaa kwa uamuzi huo ili kuona kama adhabu ya kupokonywa kwa pointi nne itabatilishwa.
Nottingham Forest ni klabu ya pili kukatwa pointi msimu huu baada ya Everton kupokwa pointi 10 mapema msimu huu kwa kukiuka kanuni za faida za Ligi ya Premia.