Kobbie Mainoo azungumza baada ya kuichezea Uingereza mara ya kwanza ilipochapwa 0-1 na Brazil

Kiungo huyo wa Man U alisema ni hisia ya kipekee ambayo hatasahau kucheza mchezo wake wa kwanza kwa England.

Muhtasari

•Mainoo alifurahi kucheza mechi yake ya kwanza ya kimataifa siku ya Jumamosi usiku wakati Uingereza iliposhindwa 0-1 na Brazil.

•Uingereza  ilishindwa 0-1 na Brazil katika mechi ya kirafiki iliyochezwa kwenye Uwanja wa W embley mwendo wa saa nne usiku wa Jumamosi.

alichezea Uingereza mara ya kwanza Jumamosi, Machi 23, 2024.
Kobbie Mainoo alichezea Uingereza mara ya kwanza Jumamosi, Machi 23, 2024.
Image: X// ENGLAND

 Mchezaji chipukizi wa Manchester United, Kobbie Mainoo alifurahi kucheza mechi yake ya kwanza ya kimataifa siku ya Jumamosi usiku wakati Uingereza iliposhindwa 0-1 na Brazil.

Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 18 alitambulishwa uwanjani katika dakika ya 75 akichukua nafasi ya kiungo wa Chelsea Connor Galagher. Hata hivyo hakuweza kuisaidia timu yake kuepuka kipigo cha aibu kwenye Uwanja wa Wembly.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa mchuano huo wa kirafiki, Mainoo alisema ni hisia ya kipekee ambayo hatasahau kucheza mchezo wake wa kwanza kwa England.

"Ni hisia maalum nikianza kucheza kimataifa kwa mara ya kwanza Wembley na mbele ya familia yangu," Mainoo alisema.

Aliongeza, "Ni wakati ambao sitasahau kamwe.”

Uingereza  ilishindwa 0-1 na Brazil katika mechi ya kirafiki iliyochezwa kwenye Uwanja wa W embley mwendo wa saa nne usiku wa Jumamosi.

Mshambulizi Endrick mwenye umri wa miaka 17 ambaye kwa sasa anachezea Palmeiras alifunga bao pekee katika mechi hiyo katika dakika ya 80 na kuipa timu yake ushindi.

Lilikuwa bao la kwanza la kimataifa kwa mchezaji huyo mwenye kipaji ambaye anatarajiwa kujiunga na Real Madrid msimu ujao.

Beki wa Manchester City Kyle Walker naye hata hakumaliza kucheza kipindi cha kwanza kwani aliumia katika dakika ya 20 na kulazimika kutolewa nje ya uwanja.

Akizungumzia jeraha hilo, kocha wa Uingereza Gareth Southgate alisema wanajipanga kumtathmini ili kubaini kama ni mbaya sana.

“Bado hatujui. Anahisi kitu lakini yeye si mchezaji ambaye anaumia mara kwa mara kwa hivyo hana uhakika kabisa ni nini. Kwa hivyo ni jambo ambalo tunapaswa kutathmini katika siku zijazo," Southgate alisema.