The Blues wanyolewa kichwa bila maji ugani Emirates

Ilikuwa ni kipindi cha pili ambapo Wanabunduki walionyesha ukali wa risasi zao huku wakifunga mabao manne zaidi.

Muhtasari

•Vijana wa Mauricio Pochettino walishindwa kufunga bao lolote huku wapinzani wao wa usiku wa Jumanne wakifunga mabao matano.

•Ushindi wa Jumanne jioni uliwapeleka vijana wa Mikel Arteta kileleni mwa jedwali wakiwa na pointi 77 na pia kuboresha tofauti yao ya mabao.

Image: INSTAGRAM// ARSENAL

Klabu ya soka ya Chelsea ilipata kichapo kikubwa na chungu kutoka kwa wapinzani wao wakubwa Arsenal katika mechi ya kusisimua iliyochezwa kwenye Uwanja wa Emirates jijini London, Uingereza siku ya Jumanne usiku.

Vijana wa Mauricio Pochettino walishindwa kufunga bao lolote huku wapinzani wao wa usiku wa Jumanne wakifunga mabao matano dhidi ya kipa Djordje Petrovic.

Mchezaji wa Kimataifa wa Ubelgiji Leandro Trossard alifunga bao la kwanza la  Wanabunduki dakika nne tu baada ya mchuano kuanza.

Timu zote zilipata nafasi kadhaa za kufunga katika dakika zilizosalia za kipindi cha kwanza lakini hakuna hata mmoja wao aliyebadilisha nafasi hizo kuwa mabao.

Ilikuwa ni kipindi cha pili ambapo Wanabunduki walionyesha ukali wa risasi zao huku wakifunga mabao manne zaidi na kuwashinda majirani zao jijini London.

Mshambulizi wa zamani wa Chelsea, Kai Harvetz na beki wa kulia wa Uingereza, Ben White walifunga mabao mawili kila mmoja na kuipa Arsenal ushindi muhimu wakati wanapigania kombe la EPL 2023/34 na Manchester City na Liverpool.

Ushindi wa Jumanne jioni uliwapeleka vijana wa Mikel Arteta kileleni mwa jedwali wakiwa na pointi 77 na pia kuboresha tofauti yao ya mabao.

Manchester City hata hivyo wana michuano miwili ambayo hawajacheza ambayo inaweza kuwapeleka kileleni mwa jedwali iwapo watashinda.

 Kwa upande wao, Liverpool wana mchuano mmoja ambao haujachezwa na ushindi utawafanya wao na Arsenal kuwa sawa kwa pointi.