Mbio za ubingwa wa EPL zachacha huku msimu ukikaribia kuisha, Sheffield yashuka daraja

Mkiani mwa jedwali, vita ya kusalia kwenye EPL pia ni kali huku Sheffield United ikiwa tayari imeshuka daraja.

Muhtasari

•Mbio za kuwania kombe la EPL zinaendelea kupamba moto huku  Arsenal na Man City kwa sasa zikionekana kuwa vinara wa kushinda kombe la mwaka huu.

•Nottingham (pointi 26), Luton Town (pointi 25) na Burnley (pointi 24) zote zinapambana kuona ni nani atanusurika kushuka daraja huku zote zikiwa bado na mechi tatu za kucheza.

Mikel Arteta, Pep Guardiola, Jurgen Klopp
Image: HISANI

Mbio za kuwania kombe la Ligi Kuu ya Uingereza zinaendelea kupamba moto huku timu mbili, Arsenal na Manchester City kwa sasa zikionekana kuwa vinara wa kushinda kombe la mwaka huu.

Liverpool pia wamo kwenye kinyang'anyiro hicho lakini juhudi zao zimeshuka katika mechi chache zilizopita, wakiwa wametoka sare katika mchuano uliopita dhidi ya West Ham.

Huku zikiwa zimesalia wiki tatu pekee kukamilika kwa msimu wa EPL 2023/24, wanabunduki ambao pia wamepewa jina la utani ‘ndovu’ kwa sasa wamekaa kileleni mwa jedwali wakiwa na pointi 80, wakiwa wamecheza jumla ya mechi 35. Wamebaki na mechi tatu za kucheza.

Washindi wa EPL 2022/23, Manchester City, wanafuatia kwa karibu katika nafasi ya pili wakiwa na jumla ya pointi 79.

Vijana wa Pep Guardiola hata hivyo wamecheza mechi chache kwani bado wana mechi nne za kucheza. Hii ina maana kwamba wanaweza kupita Arsenal ikiwa watashinda mechi zao zote

Liverpool wameshinda mechi moja pekee kati ya tano zilizopita za Premier League, matokeo ambayo yamewafanya kushuka hadi nambari tatu wakiwa na pointi 75.  Wamesalia na mechi tatu pekee za kucheza.

Arsenal itacheza dhidi ya Bournemouth katika mechi yao ijayo kwenye uwanja wa Emirates, kabla ya kufunga safari hadi Old Trafford kumenyana na Manchester United, na baadaye kucheza dhidi ya Everton nyumbani kwa mechi yao ya mwisho.

Manchester City kwa upande mwingine itamenyana na Wolves kwenye uwanja wa Etihad katika mechi ijayo, kabla ya kukutana na Fulham baadaye kucheza dhidi ya Tottenham Hotspur ugenini na hatimaye kumenyana na West Ham kwa mechi ya mwisho.

Kwa upande wao, Liverpool itacheza na Tottenham ijayo, kabla ya kumenyana na Aston Villa na Wolves kwa mechi ya mwisho.

Mkiani mwa jedwali, vita ya kusalia kwenye EPL pia ni ngumu huku Sheffield United ikiwa tayari imeshuka daraja.

Nottingham (pointi 26), Luton Town (pointi 25) na Burnley (pointi 24) zote zinapambana kuona ni nani atanusurika kushuka daraja huku zote zikiwa bado na mechi tatu za kucheza.