Mesut Ozil atangaza sapoti kwa Tottenham, atoa ahadi kubwa iwapo watashinda

Asilimia kubwa ya mashabiki wa Tottenham kwa upande wao wamesema afadhali wapoteze mechi hiyo.

Muhtasari

•Asilimia kubwa ya mashabiki wa Arsenal wanawasapoti wapinzani wao wa muda mrefu kushinda mchezo wao wa pili wa mwisho

•Kai Havert pia alitangaza kuwasapoti wapinzani wao wakuu katika mechi yao dhidi ya mshindi wa EPL 2022/23.

Mesut Ozil
Image: HISANI

Staa wa zamani wa Arsenal Mesut Ozil ametangaza kuiunga mkono klabu ya Tottenham Hotspurs kabla ya mechi yao inayosubiriwa kwa hamu dhidi ya mabingwa watetezi Manchester City.

Spurs wanatazamiwa kuwakaribisha vijana wa Pep Guardiola katika uwanja wa Tottenham Hotspurs siku ya Jumanne jioni na matokeo yatakuwa muhimu sana kwa timu  mbili zilizoketi kileleni mwa jedwali. Ikiwa Man City itashinda, itarejea kileleni mwa jedwali. Kwa upande mwingine, ikiwa Tottenham itashinda, Man City itasalia katika nafasi ya pili na kutumaini Arsenal itapoteza mechi yao ya mwisho.

Katika tweet ya Jumanne mchana, Ozil aliweka wazi kuwa anaunga mkono Tottenham kushinda na hata akaahidi kuacha kuwakejeli ikiwa hawatashindwa.

“Mara ya kwanza usiku huu: C’MON SPURSSS!!!" Ikiwa Tottenham hawatapoteza mchezo huu, sitawafanyia mzaha tena, naahidi,” Ozil alisema.

Haya yanajiri wakati asilimia kubwa ya mashabiki wa Arsenal wanawaunga mkono wapinzani wao wa muda mrefu kushinda mchezo wao wa pili wa mwisho wa EPL msimu wa 2023/24.

Cha ajabu ni kwamba, idadi kubwa ya mashabiki wa Tottenham  kwa upande wao wamesema afadhali wapoteze mechi hiyo kuliko kutoa nafasi kwa Arsenal kushinda ligi.

Siku ya Jumapili, kiungo wa kati wa Arsenal Kai Havert pia alitangaza kuwasapoti wapinzani wao wakuu katika mechi yao dhidi ya mshindi wa EPL 2022/23.

"Nitakuwa shabiki mkubwa wa Tottenham milele, sote tutakuwa. Kwa hivyo, wacha tuwe na matumaini ya bora, "Havertz alisema kwenye mahojiano.

Man City watakuwa na matumaini ya kuwapita Arsenal kwa kuwafunga Tottenham ugenini Jumanne jioni huku wanabunduki wakitumai majirani zao watasimamisha mshindani wao mkuu msimu huu.