Barcelona wamteua aliyekuwa kocha wa Bayern Munich baada ya kumtimua Xavi

Flick, ambaye alitimuliwa na Ujerumani Septemba 2023, anachukua nafasi ya Xavi, ambaye alitimuliwa wiki iliyopita.

Muhtasari

•Miamba hao wa Uhispania walitangaza uteuzi wa Flick siku ya Jumatano, siku chache tu baada ya kuondoka kwa Xavi.

•Xavi, ambaye alifutwa kazi  wiki iliyopita alisema mrithi wake "atateseka" katika nafasi hiyo.

wamemteua Hansi Flick kuwa meneja mpya.
Barcelona wamemteua Hansi Flick kuwa meneja mpya.
Image: HISANI

Sasa ni rasmi kwamba meneja wa zamani wa Bayern Munich na timu ya taifa ya Ujerumani Hansi Flick ndiye anachukua mikoba ya kuinoa Barcelona.

Miamba hao wa Uhispania walitangaza uteuzi wa Flick siku ya Jumatano, siku chache tu baada ya kuondoka kwa Xavi.

Kocha huyo mwenye umri wa miaka 59 sasa ataisimamia Barca hadi Juni 2026 baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili na klabu hiyo.

"FC Barcelona na Hansi Flick wamefikia makubaliano kwa Mjerumani huyo kuwa kocha wa timu ya kwanza ya soka ya wanaume hadi 30 Juni 2026. Kocha mpya ametia saini mkataba katika ofisi za Klabu akifuatana na rais wa FC Barcelona Joan Laporta; makamu wa kwanza wa rais anayehusika na eneo la michezo, Rafa Yuste na mkurugenzi wa michezo wa Klabu, Anderson Luís de Souza, Deco," Barcelona ilisema katika taarifa Jumatano.

Flick, ambaye alitimuliwa na Ujerumani mnamo Septemba 2023, anachukua nafasi ya Xavi, ambaye alitimuliwa wiki iliyopita.

Hapo awali aliiongoza Bayern Munich kushinda mataji matatu mwaka 2020, akishinda Bundesliga, Kombe la Ujerumani na Ligi ya Mabingwa.

Mshambulizi wa Barcelona Robert Lewandowski mwenye umri wa miaka 35 alicheza chini ya Flick katika Allianz Arena kwa misimu miwili.

Siku chache zilizopita, kocha aliyeondoka Barcelona Xavi, ambaye alifutwa kazi mwezi mmoja baada ya klabu hiyo kuthibitisha kuwa atasalia, alisema mrithi wake "atateseka" katika nafasi hiyo.

Kiungo huyo wa zamani aliiwezesha Barcelona kutwaa La Liga na kutwaa ubingwa wa Spanish Super Cup katika msimu wake wa kwanza kamili wa kuinoa klabu hiyo lakini msimu huu miamba hao wa Uhispania walimaliza pointi 10 nyuma ya mabingwa wa La Liga, Real Madrid.