Kenya Polisi Bullets watawazwa mabingwa wa 2023/24 Ligi Kuu ya Wanawake

Kenya Police Bullets pia ilimaliza msimu wa 2023/2024 bila kushindwa.

Muhtasari

•Kenya Police Bullets sasa wataelekeza nguvu zao kwenye mechi za kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa Afrika, Cecafa zinazotarajiwa kufanyika Agosti nchini Ethiopia.

•Mabingwa wa zamani Vihiga Queens, ambao walifugwa mabao 4 kwa 1 na Wadadia, walimaliza katika nafasi ya tatu kwa alama 44 sawa na Ulinzi.

Kenya Polisi Bullets wakisherehekea taji lao
Image: FKF

Kenya Police Bullets Jumatano ilitawazwa rasmi mabingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake ya 2023/2024 baada ya kuwalaza Bunyore Starlets 3-0 katika mechi ya kumalizia msimu iliyochezwa katika uwanja wa Jomo Kenyatta Mamboleo mjini Kisumu.

Ni taji lao la kwanza tangu kubadilishwa jina kutoka Thika Queens, na walikuwa wametangazwa mabingwa wakiwa na mechi iliyosalia Mei 25.

Timu hiyo inayonolewa na kocha Beldine Odemba ilitawazwa washindi baada kumaliza kwa pointi 49 baada ya raundi 22, pointi tano juu ya Ulinzi Starlets na mabingwa wa zamani Vihiga Queens mtawalia.

Ulinzi Starlets wamemaliza msimu huu katika nafasi ya pili wakiwa na 44 baada ya kuwafunga Bungoma Queens 10-0 uwanjani Ulinzi Sports Complex jijini Nairobi.

Mabingwa wa zamani Vihiga Queens, ambao walifugwa mabao 4 kwa 1 na Wadadia, walimaliza katika nafasi ya tatu kwa alama 44 sawa na Ulinzi na tofauti ya mabao.

Mechi kati ya Kibera Soccer Ladies na Madira Soccer Assassins iliyokuwa ichezwe katika uwanja wa Wolves Den huko Kajiado iliahirishwa kwa sababu za kiusalama na kupangwa tena katikati ya wiki ijayo.

Kenya Police Bullets pia ilimaliza msimu wa 2023/2024 bila kushindwa.

Kenya Police Bullets sasa wataelekeza nguvu zao kwenye mechi za kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa Afrika, Cecafa zinazotarajiwa kufanyika Agosti nchini Ethiopia.

Wakati huo huo, timu itakayoshuka daraja hadi Ligi Kuu ya Kitaifa ya Wanawake ya FKF ya 2023/24 kati ya Soccer Assassins na Zetech Sparks italazimika kusubiri hadi Jumamosi, Juni 29, 2024.