Droo ya kufuzu AFCON U20 ukanda wa CECAFA yatolewa

Kenya iko kwenye kundi A na Tanzania, Sudan, Rwanda na Djibouti.

Muhtasari

• Mechi za kufuzu AFCON ya wavulana chini ya umri wa miaka 20 itaandaliwa Tanzania kuanzia Oktoba 6 hadi Oktoba 20.

Junior Stars
Image: TWITTER// ABABU NAMWAMBA

Droo ya mechi za kufuzu AFCON ya wavulana wasiozidi umri wa miaka 20 katika baraza la vyama vya soka Afrika mashariki na kati CECAFA imetolewa.

Droo hiyo imefanyika jijini Dar es Salaam, Tanzania. Kipute hicho cha AFCON U-20 kitaandaliwa  nchini Tanzania kuanzia Oktoba tarehe 6 hadi Oktoba 20 mwaka huu.

Timu ya taifa ya Kenya maarufu kama Rising Stars imewekwa kundi A na Taifa Stars ya wenyeji Tanzania, Rwanda, Sudan na Djibouti. 

Mabingwa watetezi wa CECAFA U-20 Uganda imewekwa katika kikapu kimoja cha kundi B watakapomenyana na Sudan Kusini, Ethiopia na Burundi.

Mechi hizo za kufuzu zitakazochezwa nchini Tanzania, zitawapa washindi katika kila kundi tiketi ya kucheza AFCON ya 2025.

Nchi itakayoandaa mashindano hayo ya mwaka 2025, itatajwa wakati wa kikao cha mkutano mkuu wa waandalizi wa AFCON.

Mkutano huo utaandaliwa Oktoba 10 2024 jijini Kinshasa, jiji kuu la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Uwanja wa Azam Complex, uga wa KMC na uwanja wa Major General Isamuhyo zitatumika kuanzia Oktoba 6 kwa mechi za kufuzu AFCON 2025 kwa timu za ukanda wa CECAFA.

Timu mbili zitakazofika fainali ya CECAFA zitawakilisha Afrika Mashariki na kati katika AFCON ya 2025.