Kenya ndio timu katika kundi letu tunaogopa, asema Onana

Harambee Stars inaongoza msimamo wa jedwali kundi J

Muhtasari

• Cameroon imecheza mechi mbili ambapo imeshinda dhidi ya Namibia na kutoka sare na Zimbabwe

Kipa wa Manchester United Andre Onana
Image: MAKTABA

Golkipa wa timu ya taifa ya Cameroon na Manchester United Andrea Onana amesema kuwa Harambee Stars ndio timu anaogopa kukutana nayo katika  mechi za kufuzu kwa dimba la AFCON.

Onana alisema haya katika mkutano na waandishi wa habari katika video inayosambaa mtandaoni baada ya mechi yao dhidi ya Zimbabwe iliyotaka sare ya kutofungana.

Cameroon ipo katika kundi J pamoja na Kenya, Zimbabwe na Namibia.

Kufikia sasa, timu zote katika kundi J zimecheza mechi mbili na Harambee Stars ya Kenya inaongoza msururu wa jedwali hilo kwa alama nne. Cameroon ni ya pili kwa alama sawia ila Kenya ina wingi wa mabao.

"Kenya ndio timu pekee katika kundi letu inayotupa ushindani mkali lakini tunatumai tutafika hatua ya kufuzu." Alisema Onana.

Harambee Stars itacheza na Indomitable Lions ya Cameroon mechi ya tatu ya kundi J tarehe 7 Oktoba, 2024 kabla ya kuwakaribisha hao hao Cameroon tarehe 15 Oktoba, 2024 mechi ya mkondo wa pili.