Bodi ya uchaguzi wa FKF yazinduliwa jijini Nairobi

Uchaguzi wa FKF unatarajiwa kufanyika hivi karibuni kupisha usimamizi mpya kwa minne ijayo

Muhtasari

• Bodi ya uchaguzi yenye wanachama 5 imezinduliwa kuendesha uchaguzi wa shirikisho la soka nchini fkf.

• Aliyekuwa mwenyekiti wa AFC Leopards Dan Mule ni mwanachama katika bodi hiyo pamoja na rais wa chama cha wanahabari wa michezo nchini.

Nembo ya shirikisho la soka nchini FKF
Nembo ya shirikisho la soka nchini FKF
Image: FKF

Bodi itakayosimamia uchaguzi wa shirikisho la soka nchini Kenya FKF imezinduliwa katika hafla iliyoandaliwa hotelini Kempinski jijini Nairobi.

Bodi hiyo yenye wanachama watano imetwikwa jukumu la kusimamia uchaguzi wa utawala mpya wa FKF kwa miaka minne ijayo .Uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika hivi karibuni.

FKF imekuwa chini ya rais Nick Mwendwa ambaye amehudumu kwa zaidi ya miaka minane katika awamu mbili.

Kwenye bodi mpya, Hesborn Owilla ambaye ni mtafiti wa mawasiliano na vyombo vya habari ndiye mwenyekiti na Merceline Sande akihudumu katika nafasi ya katibu wa bodi.

Wanachama wengine ni rais wa chama cha waandishi wa habari za michezo nchini (SJAK) James Waindi, mwenyekiti wa zamani wa AFC Leopards Dan Mule na Alfred Ng'ang'a.

Baada ya kuzinduliwa kwao, mwenyekiti Owilla alisema kuwa  bodi hiyo itahakikisha uchaguzi unaotarajiwa utakuwa uchaguzi huru, wa haki na wa kuthibitishwa.

"Huo uchaguzi utajenga msingi wa mchezo wetu, mchezo ambao mashabiki,wachezaji na washikadau wametuamini tuulinde."  Alisema Owilla.

Vile vile, mwenyekiti huyo amehakikishia washikadau wa soka kuwa bodi hiyo kwa pamoja wamejitolea kufanya uchaguzi na kutoa matokeo ambayo kila mtu atajivunia.

Owilla na wenzake wamepewa ofisi ambayo wataendesha shughuli za bodi hiyo katika jumba la Kandanda.

Bodi hiyo pia katika siku zijazo inatarajiwa kutangaza tarehe rasmi ya kuandaliwa kwa uchaguzi sawia na mwelekeo wa jinsi uchaguzi huo utaendeshwa .