Arsenal yaomboleza baada ya mchezaji wake wa zamani kuzirai na kufariki wakati akicheza

Klabu ya Arsenal imeomboleza kifo cha mchezaji wake wa zamani Fabian Caballero.

Muhtasari

•Katika taarifa fupi ya Jumamosi mchana, Arsenal FC ilibainisha kuwa kila mmoja katika klabu hiyo amehuzunishwa na kifo cha Caballero.

•Kifo cha Caballero kinakuja baada ya kuzirai akicheza futsal na marafiki zake katika mji mkuu wa nchi hiyo Asuncion.

Image: HISANI

Klabu ya Arsenal imeomboleza kifo cha mchezaji wake wa zamani Fabian Caballero.

Mshambulizi huyo wa zamani wa Paraguay ambaye aliichezea Arsenal mechi kadhaa katika msimu wa 1998-99 anaripotiwa kufariki Jumamosi akiwa na umri wa miaka 46.

Katika taarifa fupi ya Jumamosi mchana, Arsenal FC ilibainisha kuwa kila mmoja katika klabu hiyo amehuzunishwa na kifo cha Caballero,.

"Kila mmoja katika klabu amehuzunishwa sana kusikia kifo cha ghafla cha mchezaji wetu wa zamani, Fabian Caballero. Mawazo yetu yako kwa familia yake na marafiki wakati huu," Arsenal ilisema.

Ripoti kutoka nchini Paraguay zinasema kifo cha Caballero kinakuja baada ya kuzirai akicheza futsal na marafiki zake katika mji mkuu wa nchi hiyo Asuncion.

"Shirikisho la Soka la Paraguay linasikitika sana kuondokewa na mwanasoka wa zamani, Fabian Caballero, ambaye alikuwa na taaluma bora katika soka ya Paraguay na nje ya nchi," Shirikisho la Soka la Paraguay lilisema katika taarifa.

Baada ya kuzaliwa Argentina, Caballero alitumia miaka yake ya ujana huko Paraguay ambapo alianza taalumi yake kabla ya kuhamia London kaskazini kwa mkopo.

 Caballero alicheza mechi yake ya kwanza ya Ligi ya Premia dhidi ya Middlesbrough akichukua nafasi ya Freddie Ljungberg lakini alitumia muda zaidi katika kikosi cha akiba cha Arsenal akishirikiana na Nwankwo Kanu wakati huo.