Beki wa zamani wa Barcelona Dani Alves azuiliwa kwa madai ya unyanyasaji wa kingono

Alves anadaiwa kumyanyasa mwanamke kwa kumgusa sehemu ya mwili wake kwa namna isiyofaa.

Muhtasari

•Dani Alves anashikiliwa katika kwa muda gerezani huku akisubiri uchunguzi kuhusiana na madai ya unyanyasaji wa kingono yanayomkabili.

Dani Alves
Image: BBC

Mlinzi wa Brazil Dani Alves anashikiliwa katika kwa muda gerezani huku akisubiri uchunguzi kuhusiana na madai ya unyanyasaji wa kingono yanayomkabili.

Mlinzi huyo wa Barcelona, mwenye umri wa miaka 39, anadaiwa kumyanyasa mwanamke kwa kumgusa sehemu ya mwili wake kwa namna isiyofaa walipokuwa katika ukumbi wa starehe wa usiku mjini Barcelona mwezi Disemba.

Alves, ambaye alikana madai hayo, alipelekwa mahabusu na kuhojiwa na jaji mjini Barcelona Ijumaa.

Klabu yake, ya Mexico Pumas UNAM, ilikatisha mara moja mkataba wa Alves, kufuatia madai hayo.

"Klabu ilirejelea kusema kuwa haiwezi kuvumilia vitendo vya mmoja wao yeyote, hata awe nani, ambavyo vinakwenda kinyume na maadili ya klabu ," alisema rais wa mchezo wa klabu ya Pumas, Leopoldo Silva.

"Hatuwezi kuruhusu mwenendo wa mtu mmoja kuharibu falsafa ya kazi yetu, ambayo imekuwa ya mfano wa kuigwa katika kipindi chote cha historia ya klabu."

Alves aliiichezea Barcelona mara 408 na pia alikuwa sehemu ya kikosi cha Brazil katika Kombe la Dunia la 2022.

Polisi wa eneo hilo Mossos d'Esquadra amethibitisha taarifa ya kukamatwa na kufungwa kwa Alves kwa mashirika ya habari ya Reuters na AFP.