De Gea avunja kimya kuhusu Man United kutaka arejee baada ya kumfukuza vibaya

Mashetani Wekundu walikataa kumpa mkataba mpya baada ya ule wa zamani kukatika Juni mwaka huu

Muhtasari

•Kumekuwa na ripoti nyingi kwamba United wanataka kumsaini tena kipa de Gea ili kujaza nafasi ya Andre Onana akienda AFCON.

•De gea alijiunga na Mashetani Wekundu mwaka wa 2011 na alichezea klabu hiyo kwa zaidi ya muongo mmoja hadi Juni 2023.

David de Gea na nahodha wa United Bruno Fernandes
Image: TWITTER// David de Gea

Aliyekuwa kipa wa Manchester United, David de Gea ameonekana kujibu ripoti kwamba klabu hiyo yake ya zamani inamtaka arudi.

Kumekuwa na ripoti nyingi kwamba klabu hiyo ya EPL inataka kumsaini tena kipa huyo mwenye umri wa miaka 32 ili kujaza nafasi ya Andre Onana ambaye anatarajiwa kuiwakilisha nchi yake ya Cameroon wakati wa michuano ya AFCON 2024 itakayochezwa Januari mwakani.

Katika kile ambacho kilionekana kama jibu la madai hayo ya ajabu ya mambo, de Gea aliposti emoji ya 'kufikiri' ili kushiriki mawazo yake ya sasa.

",🤔" mchezaji huyo wa zamani wa kimataifa wa Uhispania aliandika kwenye akaunti yake ya mtandao wa Twitter Alhamisi mchana.

Mamia ya mashabiki wameendelea kutoa maoni yao kuhusu hisia za mlinda mlango huyo wa zamani wa Man United huku wengi wakihusisha emoji hiyo na ripoti zinazoendelea.

Ikiwa mwanasoka huyo wa miaka 32 atarejea katika Old Trafford, basi ingeonekana jambo la kushangaza sana ikizingatiwa kwamba Mashetani Wekundu walikataa kumpa mkataba mpya baada ya ule wa zamani kukatika Juni mwaka huu.

Mchezaji huyo wa Kimataifa wa Uhispania alikuwa amevuna mafanikio makubwa katika klabu hiyo ya EPL na hata alishinda tuzo ya ‘golden glove’ msimu uliopita kwa kucheza kwa idadi kubwa zaidi ya msimu bila kufungwa. Pia alisaidia timu hiyo yake kutofungwa mabao mengi ya wazi kwa takriban miaka 12 ambayo amekuwa pale.

De gea alijiunga na Mashetani Wekundu mwaka wa 2011 na alichezea klabu hiyo ya mji wa Machester kwa zaidi ya muongo mmoja hadi mkataba wake ulipoisha mwezi Juni.