Huzuni huku mchezaji wa kimataifa wa Ghana akinguka na kufariki uwanjani wakati wa mechi

Dwamena anaripotiwa kupatwa na mshtuko wa moyo akiwa anacheza uwanjani , hali iliyopelekea kifo chake cha ghafla.

Muhtasari

•Dwamena, 28, alifariki baada ya kuzimia uwanjani wakati kwa mchuano baina ya KF Egnatia na Partizani siku ya Jumamosi.

•Mchuano huo ulisimamishwa mara moja ukiwa 1-1 na haukuendelea tena.

Marehe,mu Raphael Duamena
Image: HISANI

Waghana wanaomboleza kifo cha mmoja wa washambuliaji bora kuwakilisha taifa hilo katika mashindano ya kimataifa, Raphael Dwamena aliyekata roho siku ya Jumamosi.

Dwamena, 28, anaripotiwa kufariki dunia nchini Albania baada ya kuzimia uwanjani wakati kwa mchuano baina ya klabu yake ya KF Egnatia na Partizani siku ya Jumamosi.

Ripoti zinaashiria kuwa mchezaji huyo wa zamani wa Levante alipatwa na mshtuko wa moyo akiwa anacheza uwanjani, hali iliyopelekea kifo chake cha ghafla.

"Shirikisho ya Soka ya Ghana inasikitika kusikia kifo cha mchezaji wetu wa zamani Raphael Dwamena na tungependa kutoa rambirambi zetu kwa familia yake katika wakati huu mgumu," Shirikisho ya Soka ya Ghana (GFA) ilimuomboleza Dwamena katika taarifa.

Ilisema zaidi, "Mshambuliaji huyo wa zamani wa Ghana alitangazwa kuwa amefariki Jumamosi baada ya kuanguka kwenye uwanja wa mpira wakati wa mechi ya Ligi nchini Albania."

Video zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha mchezaji huyo akianguka uwanjani peke yake katika dakika ya 24 ya mechi kati ya Egnatia na Partizani.

Wachezaji wengine waliokuwa uwanjani walikimbia kuona kilichotokea na kujaribu kusaidia lakini licha ya kuingilia kati kwa wahudumu wa afya mara moja, Shirikisho la Soka la Albania lilisema 'mchezaji huyo kwa bahati mbaya aliaga dunia.'

Mchuano huo ulisimamishwa mara moja ukiwa 1-1 na haukuendelea tena.

Dwamena ndiye aliyekuwa anaongoza kwa ufungaji mabao katika Ligi Kuu ya Albania msimu huu akiwa amefunga mabao tisa kabla ya kifo chake cha bahati mbaya.

Marehemu alikuwa amewakilisha timu ya taifa ya Ghana mara tisa na alikuwa amefunga mara mbili. Hapo awali aliwahi pia kucheza katika nchi mbalimbali zikiwemo Uhispania, Denmark na Uswizi.

Mshambulizi huyo hapo awali alikuwa amekumbwa na matatizo ya moyo, ikiwa ni pamoja na wakati wa mchuano wa mwaka 2021 na klabu ya soka ya Blau-Veis Linz ya Austria ambapo alihudumiwa na  kulazwa hospitalini kwa matatizo ya moyo.

Tunaitakia roho ya Dwamena mapumziko ya amani.