Jeki kwa Wanabunduki baada ya Gabriel Jesus kurejea mazoezini

Jesus alionekana akifanya mazoezi na wachezaji wengine siku ya Alhamisi asubuhi.

Muhtasari

•Gabriel Jesus tayari amerejea mazoezini na wachezaji wengine wa Arsenal, wiki kadhaa tu baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti.

•Mapema mwezi huu, Arteta alithibitisha kwamba Mbrazil huyo alifanyiwa upasuaji mdogo baada ya kusumbuliwa na goti mara kwa mara.

Image: HISANI

Mashabiki wa Arsenal sasa wanaweza kutabasamu kwani mshambuliaji wao mkuu Gabriel Jesus tayari amerejea mazoezini na wachezaji wengine wa klabu hiyo ya London, wiki kadhaa tu baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti.

Jesus alionekana akifanya mazoezi na vijana wengine wa Arteta siku ya Alhamisi asubuhi lakini klabu bado haijatoa taarifa rasmi kuhusu kurejea kwake.

Bado haijafahamika wazi ni lini mchezaji huyo wa kimataifa wa Brazil mwenye umri wa miaka 26 atakuwa katika nafasi ya kuchaguliwa kucheza tena lakini kurejea kwake mazoezini ni kiashiria kikubwa kwamba atarejea uwanjani hivi karibuni.

Mchezaji huyo wa zamani wa klabu ya Manchester City alifanyiwa upasuaji wa goti mwishoni mwa mwezi uliopita na meneja wa Arsenal Mikel Arteta alitangaza kwamba wangemkosa kwa wiki kadhaa.

Mapema mwezi huu, Arteta alithibitisha kwamba Mbrazil huyo alifanyiwa upasuaji mdogo baada ya kusumbuliwa na goti mara kwa mara.

Wakati huo, alithibitisha kuwa mshambuliaji huyo hangeweza kucheza kwa wiki kadhaa huku akiendelea kupata nafuu kutokana na utaratibu huo.

“Kwa bahati mbaya alifanyiwa upasuaji kidogo asubuhi ya leo. Alikuwa na usumbufu katika goti lake ambao umekuwa ukisababisha mashida kadhaa, na ilibidi wamchunguze na kuyasuluhisha. Sio upasuaji mkubwa lakini atakuwa nje kwa wiki chache nadhani,” Arteta aliambia wanahabari baada ya mechi ya Kombe la Emirates dhidi ya Monaco.

Mhispania huyo alibainisha kuwa ni pigo kubwa kuona Jesus akilazimika kufanyiwa upasuaji huo na kudokeza kwamba mchezaji huyo wa Kimataifa wa Brazil alikuwa ameanza kurejea katika hali yake nzuri kabla ya kupata usumbufu kwenye goti lake.

"Alikuwa katika hali nzuri lakini tumempoteza. Amekuwa akihisi usumbufu katika wiki chache zilizopita na ilibidi waangalie na tulilazimika kufanya uamuzi na bora zaidi ni kumlinda mchezaji na kumrudisha haraka iwezekanavyo. Tuliamua kufanya hivyo,” alisema.

Arteta alifichua kuwa jeraha ambalo lilimkumba mshambuliaji huyo linahusiana na jeraha la awali alilopata wakati Kombe la Dunia akiwa na taifa lake Brazil mwishoni mwa mwaka jana.

Mwezi Desemba mwaka jana, Jesus alifanyiwa upasuaji wa goti baada ya kuumia alipokuwa akiichezea Brazil katika michuano ya Kombe la Dunia la Fifa iliyofanyika nchini Qatar. Mshambulizi huyo mwenye umri wa miaka 26 alikosa sehemu kubwa ya awamu ya pili ya msimu wa 2022/23, jambo ambalo lilikuwa pigo kubwa kwa Arsenal ambao walimtegemea sana kufunga mabao.

Kwa bahati nzuri aliweza kumaliza msimu vizuri nao na hata ameshiriki katika mechi kadhaa za kujiandaa na msimu kabla ya kufanyiwa utaratibu mdogo Jumatano asubuhi.